Leviticus 5

Sadaka Nyingine Za Kuondoa Dhambi

1“ ‘Ikiwa mtu atakuwa ametenda dhambi kwa sababu hakusema alipotakiwa kutoa ushahidi hadharani kuhusu jambo aliloona au kujua habari zake, yeye anastahili adhabu.

2“ ‘Au kama mtu akigusa kitu cho chote ambacho si safi kwa kawaida ya ibada, kama ni mizoga ya wanyama pori walio najisi, au ya wanyama wafugwao walio najisi, au ya viumbe vitambaavyo ardhini, hata kama hana habari, amekuwa najisi na mwenye hatia.

3“ ‘Au kama akigusa kitu kilicho kichafu kinachotokana na binadamu, kitu cho chote kile kinachoweza kumfanya awe najisi, hata ikiwa hana habari juu yake, atakapojua atakuwa ana hatia.

4“ ‘Au kama mtu ameapa kufanya kitu cho chote bila kufikiri kikiwa chema au kibaya, kwa vyo vyote mtu aweza kuapa kwa uzembe akiwa hana habari juu yake, hata kama hatambui juu yake kwa vyo vyote, atakapofahamu atakuwa na hatia.

5“ ‘Wakati mtu ye yote atakapokuwa na hatia katika mojawapo ya haya, lazima akiri kuwa ni kwa njia gani ametenda dhambi, 6na kwa ajili ya adhabu ya dhambi aliyoitenda lazima alete kwa BWANA kondoo jike au mbuzi kutoka kwenye kundi lake kama sadaka ya dhambi; naye kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake kwa dhambi yake.

7“ ‘Lakini huyo mtu kama hataweza kumtoa mwana-kondoo, ataleta hua wawili au makinda mawili ya njiwa kwa BWANA kuwa adhabu kwa ajili ya dhambi yake, mmoja wa hao ndege kwa ajili ya sadaka ya dhambi na wa pili kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa. 8Atawaleta kwa kuhani, ambaye atamtoa kwanza huyo mmoja kwa ajili ya sadaka ya dhambi. Atamvunja shingo yake na kuacha kichwa chake kikining'inia, 9naye atanyunyiza sehemu ya hiyo damu ya sadaka ya dhambi kwenye pembe za madhabahu, damu iliyobaki lazima ichuruzwe chini ya madhabahu. Hii ni sadaka ya dhambi. 10Kisha kuhani atamtoa yule wa pili kama sadaka ya kuteketezwa kwa kufuata utaratibu uliowekwa na kufanya upatanisho kwa ajili yake kwa dhambi aliyoitenda, naye atasamehewa.

11“ ‘Ikiwa basi, hawezi kupata hua wawili au makinda mawili ya njiwa, ataleta sehemu ya kumi ya efa
5.11 Sehemu ya kumi ya efa ni sawa na kilo moja
ya unga laini kwa ajili ya sadaka ya dhambi. Kamwe asiweke mafuta wala uvumba juu yake kwa sababu ni sadaka ya dhambi.
12Atauleta kwa kuhani, naye atauchukua unga huo konzi moja kama sehemu ya kumbukumbu na atauteketeza kwenye madhabahu juu ya sadaka zilizotolewa kwa BWANA kwa moto. Hii ni sadaka ya dhambi. 13Kwa njia hii kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake kwa dhambi mojawapo ya hizo alizotenda, naye atasamehewa. Sadaka iliyobaki itakuwa ya kuhani, kama ilivyokuwa ile sadaka ya nafaka.’ ”

Sadaka Ya Hatia

14BWANA akamwambia Mose: 15“Mtu anapokiuka na kutenda dhambi pasipo kukusudia kuhusu mojawapo ya mambo matakatifu ya BWANA, huyo mtu ataleta kwa BWANA kama adhabu, kondoo dume mmoja kutoka katika kundi lake, asiye na dosari na mwenye thamani halisi kifedha, kulingana na shekeli ya mahali patakatifu. Hii ni sadaka ya hatia. 16Ni lazima alipe kwa yale aliyoshindwa kufanya kuhusu vitu vitakatifu, kwa kuongeza sehemu ya tano ya thamani ile na kuitoa yote kwa kuhani, ambaye atamfanyia upatanisho kwa huyo kondoo dume kama sadaka ya dhambi, naye atasemehewa.

17“Kama mtu akifanya dhambi na kufanya yale yaliyokatazwa katika mojawapo ya amri za BWANA, hata ikiwa hajui, yeye ana hatia na anastahili adhabu. 18Atamletea kuhani kama sadaka ya hatia kondoo dume kutoka kundi lake, kondoo asiye na dosari na mwenye thamani halisi kifedha. Kwa njia hii kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake kwa kosa alilotenda bila kukusudia, naye atasamehewa. 19Hii ni sadaka ya hatia; amekuwa na hatia kwa kufanya kosa dhidi ya BWANA.”

Copyright information for Neno