Leviticus 6

Kurudisha Kilichochukuliwa

1BWANA akamwambia Mose: 2“Kama mtu ye yote akitenda dhambi naye si mwaminifu kwa BWANA kwa kumdanganya jirani yake kuhusu kitu fulani alichokabidhiwa au kimeachwa chini ya utunzaji wake au kimeibwa, au kama akimdanganya, 3au akiokota mali iliyopotea na akadanganya au kuapa kwa uongo, au kama akitenda dhambi yo yote ambayo watu waweza kuitenda; 4wakati akitenda dhambi hizo na kuwa mwenye hatia, ni lazima arudishe kile alichokuwa amekiiba au amekichukua kwa dhuluma, au alichokuwa amekabidhiwa, au mali iliyokuwa imepotea akaipata, 5au cho chote alichokuwa amekiapia kwa uongo. Lazima akirudishe kikamilifu, aongeze sehemu ya tano ya thamani yake na kumpa vyote mwenye mali siku ile anapopeleka sadaka yake ya hatia. 6Kisha kama adhabu lazima amletee kuhani, yaani kwa BWANA, sadaka yake ya hatia, kondoo dume kutoka katika kundi asiye na dosari na mwenye thamani kamili. 7Kwa njia hii kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake mbele za BWANA, naye atasamehewa kwa kosa lo lote katika mambo hayo aliyoyatenda yaliyomfanya kuwa na hatia.”

Sadaka Ya Kuteketezwa

8BWANA akamwambia Mose: 9“Mpe Aroni na wanawe agizo hili: ‘Haya ndiyo masharti kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa: Sadaka ya kuteketezwa itabaki kwenye moto juu ya madhabahu usiku kucha, mpaka asubuhi, nao moto lazima uwe unaendelea kuwaka juu ya madhabahu. 10Kisha kuhani atavaa mavazi yake ya kitani, pamoja na nguo za kitani za ndani, kisha ataondoa majivu ya sadaka ya kuteketezwa ambayo moto umeteketeza juu ya madhabahu na kuyaweka kando ya madhabahu. 11Kisha atayavua mavazi haya na kuvaa mengine, atachukua yale majivu nje ya kambi na kupeleka mahali palipo safi kwa kawaida ya ibada. 12Moto ulio juu ya madhabahu lazima uwe unaendelea kuwaka, kamwe usizimike. Kila asubuhi kuhani ataongeza kuni na kupanga sadaka ya kuteketezwa juu ya moto na kuteketeza mafuta ya sadaka za amani juu yake. 13Moto lazima uendelee kuwaka juu ya madhabahu mfululizo, kamwe usizimike.

Sadaka Ya Nafaka

14“ ‘Haya ndiyo masharti ya sadaka ya nafaka: Wana wa Aroni wataileta mbele za BWANA, mbele za madhabahu. 15Kuhani atachukua konzi ya unga laini na mafuta, pamoja na uvumba wote juu ya sadaka ya nafaka na kuteketeza sehemu ya kumbukumbu juu ya madhabahu kama harufu nzuri ya kumpendeza BWANA. 16Aroni na wanawe watakula sehemu iliyobaki, lakini italiwa bila kutiwa chachu mahali patakatifu, wataila kwenye ua wa Hema la Kukutania. 17Kamwe haitaokwa na chachu; nimewapa kama fungu lao la sadaka iliyotolewa kwangu kwa moto. Ni takatifu sana kama vile ilivyo sadaka ya dhambi na ya hatia. 18Kila mwanaume mzao wa Aroni aweza kuila. Ni fungu lake la kawaida la sadaka zilizotolewa kwa BWANA kwa moto kwa vizazi vijavyo. Cho chote kinachozigusa kitakuwa kitakatifu.’ ”

19Tena BWANA akamwambia Mose, 20“Hii ni sadaka ambayo Aroni na wanawe wanapaswa kuleta kwa BWANA siku atakapotiwa mafuta: sehemu ya kumi ya efa
6.20 Sehemu ya kumi ya efa ni sawa na kilo moja
ya unga laini kama sadaka ya kawaida ya nafaka, nusu yake ataitoa asubuhi na nusu nyingine jioni.
21Iandae kwa mafuta kwenye kikaango; ilete ikiwa imechanganywa vizuri na utoe hiyo sadaka ya nafaka ikiwa imevunjwa vipande vipande kuwa harufu nzuri ya kumpendeza BWANA. 22Mtoto atakayeingia mahali pake kama kuhani aliyetiwa mafuta ndiye atakayeiandaa. Ni fungu la kawaida la BWANA, nalo litateketezwa kabisa. 23Kila sadaka ya nafaka ya kuhani itateketezwa kabisa; kamwe haitaliwa.”

Sadaka Ya Dhambi

24BWANA akamwambia Mose, 25“Mwambie Aroni na wanawe: ‘Haya ndiyo masharti kwa ajili ya sadaka ya dhambi: Sadaka ya dhambi itachinjwa mbele za BWANA mahali sadaka ya kuteketezwa ichinjiwapo, ni takatifu sana. 26Kuhani anayeitoa ndiye atakayeila, italiwa mahali patakatifu, katika ua wa Hema la Kukutania. 27Cho chote kitakachogusa nyama yo yote ya hiyo sadaka kitakuwa kitakatifu na kama hiyo damu itadondokea juu ya vazi, lazima uifulie mahali patakatifu. 28Chungu cha udongo kitakachopikiwa nyama lazima kivunjwe, lakini kama imepikiwa kwenye chombo cha shaba, chombo hicho kitasuguliwa na kusuuzwa kwa maji. 29Kila mwanaume katika familia ya kuhani aweza kula nyama hiyo, ni takatifu sana. 30Lakini kila sadaka ya dhambi ambayo damu yake imeletwa ndani ya Hema la Kukutania kufanya upatanisho katika Mahali Patakatifu kamwe haitaliwa; lazima iteketezwe.

Copyright information for Neno