Malachi 1

1Ujumbe: Neno la BWANA kwa Israeli kupitia kwa Malaki.

Yakobo Alipendwa, Esau Alichukiwa

2BWANA asema, “Nimewapenda ninyi.”

“Lakini ninyi mnauliza, ‘Wewe umetupendaje?’ ”

BWANA asema, “Je, Esau hakuwa ndugu yake Yakobo? Hata hivyo nimempenda Yakobo,
3lakini nikamchukia Esau, nami nimeifanya milima yake kuwa ukiwa na urithi wake nimewapa mbweha wa jangwani.”

4Edomu anaweza kusema, “Ingawa tumepondwapondwa, tutajenga upya magofu.”

Lakini hili ndilo BWANA Mwenye Nguvu Zote asemalo: “Wanaweza kujenga, lakini nitabomoa. Wataitwa Nchi Ovu, watu ambao siku zote wapo chini ya ghadhabu ya BWANA.
5Mtayaona kwa macho yenu wenyewe na kusema, ‘BWANA ni mkuu, hata nje ya mipaka ya Israeli!’

Dhabihu Zilizo Na Mawaa

6“Mwana humheshimu baba yake, naye mtumishi humheshimu bwana wake. Kama mimi ni baba, iko wapi heshima ninayostahili? Kama mimi ni bwana, iko wapi heshima ninayostahili?” asema BWANA Mwenye Nguvu Zote. “Ni ninyi, Enyi makuhani, mnaolidharau Jina langu.

“Lakini mnauliza, ‘Tumelidharau Jina lako kwa namna gani?’

7“Mnatoa sadaka chakula kilichotiwa unajisi juu ya madhabahu yangu.

“Lakini ninyi mnauliza, ‘Tumekutia unajisi kwa namna gani?’

“Kwa kusema kuwa meza ya BWANA ni ya kudharauliwa.
8Wakati mletapo dhabihu wanyama walio vipofu, je, hilo si kosa? Mnapoleta dhabihu zilizo vilema au wanyama wagonjwa, je, hilo si kosa? Jaribuni kuvitoa kwa mtawala wenu! Je, angefurahiwa nanyi? Je, atawakubalia?” Asema BWANA Mwenye Nguvu Zote.

9“Basi mwombeni Mungu awe na neema kwetu. Je, kwa sadaka kama hizo kutoka mikononi mwenu, atawapokea?” Asema BWANA Mwenye Nguvu Zote.

10“Laiti mmoja wenu angalifunga milango ya Hekalu, ili msije mkawasha moto usiokuwa na faida juu ya madhabahu yangu! Sina furaha nanyi,” asema BWANA Mwenye Nguvu Zote, “nami sitaikubali sadaka toka mikononi mwenu. 11Jina langu litakuwa kuu miongoni mwa mataifa, kuanzia maawio ya jua hata machweo yake. Kila mahali uvumba na sadaka safi zitaletwa kwa Jina langu, kwa sababu Jina langu litakuwa kuu miongoni mwa mataifa,” asema BWANA Mwenye Nguvu Zote.

12“Lakini mnalinajisi Jina langu kwa kusema kuhusu meza ya Bwana, ‘Imetiwa unajisi pamoja na chakula chake. Ni ya kudharauliwa.’ 13Nanyi mnasema, ‘Mzigo gani huu!’ Nanyi mnaidharau kwa kiburi,” asema BWANA Mwenye Nguvu Zote.

“Wakati mnapowaleta wanyama mliopokonya kwa nguvu, vilema au walio wagonjwa na kuwatoa kama dhabihu, je, niwakubali kutoka mikononi mwenu?” asema BWANA.
14“Amelaaniwa yeye adanganyaye aliye na mnyama wa kiume anayekubalika katika kundi lake na kuweka nadhiri ya kumtoa, lakini akatoa dhabihu ya mnyama aliye na dosari kwa BWANA. Kwa kuwa mimi ni Mfalme Mkuu, nalo Jina langu linapaswa kuogopwa miongoni mwa mataifa,” asema BWANA Mwenye Nguvu Zote.

Copyright information for Neno