Mark 1

Mahubiri Ya Yohana Mbatizaji

Mwanzo wa Injili ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu.

Kama ilivyoandikwa katika kitabu cha nabii Isaya: “Tazama, namtuma mjumbe wangu mbele yako,
yeye atakayeitengeneza njia yako”:
“sauti ya mtu aliaye nyikani.
‘Itengenezeni njia ya Bwana,
yanyosheni mapito yake.’ ”


Yohana alikuja, akibatiza huko nyikani, akihubiri ubatizo wa toba kwa ajili ya ondoleo la dhambi. Watu kutoka Uyahudi wote na sehemu zote za Yerusalemu walikuwa wakimwendea, naye akawabatiza katika Mto Yordani, wakitubu dhambi zao. Yohana alivaa mavazi yaliyotengenezwa kwa singa za ngamia na mkanda wa ngozi kiunoni mwake. Chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwitu. Naye alihubiri akisema, “Baada yangu atakuja yeye aliye na uwezo kuliko mimi, ambaye sistahili hata kuinama na kulegeza kamba za viatu vyake. Mimi nawabatiza kwa maji, lakini yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu.”

Ubatizo Wa Yesu

Wakati huo Yesu akaja kutoka Nazareti ya Galilaya, naye akabatizwa na Yohana katika Mto Yordani. 10 Yesu alipokuwa akitoka ndani ya maji, aliona mbingu zikifunguka na Roho akishuka juu yake kama hua. 11 Nayo sauti kutoka mbinguni ikasema, “Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu, ambaye nimependezwa nawe.”

Majaribu Ya Yesu

12 Wakati huo huo, Roho akamwongoza Yesu kwenda nyikani, 13 naye akawa huko nyikani kwa muda wa siku arobaini, akijaribiwa na Shetani. Alikaa na wanyama wa mwituni, nao malaika wakamhudumia.

Yesu Aanza Kuhubiri

14 Baada ya Yohana kukamatwa na kutiwa gerezani, Yesu aliingia Galilaya akaanza kuhubiri habari njema ya Mungu, 15 akisema, “Wakati umewadia, Ufalme wa Mungu umekaribia. Tubuni na kuiamini Habari Njema.”

Yesu Awaita Wanafunzi Wanne

16 Yesu alipokuwa akitembea kandokando ya Bahari ya Galilaya alimwona Simoni na Andrea nduguye wakizitupa nyavu zao baharini, kwa kuwa hawa wawili walikuwa wavuvi. 17 Yesu akawaambia, “Njoni nifuateni, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu.” 18 Mara wakaacha nyavu zao, wakamfuata Yesu.

19 Alipokwenda mbele kidogo, akamwona Yakobo mwana wa Zebedayo na Yohana nduguye, wakiwa kwenye mashua yao wakizitengeneza nyavu zao. 20 Papo hapo akawaita, nao wakamwacha Zebedayo baba yao kwenye mashua pamoja na watumishi wa kuajiriwa, nao wakamfuata Yesu.

Yesu Amtoa Pepo Mchafu

21 Wakaenda mpaka Kapernaumu. Ilipofika siku ya Sabato, mara Yesu akaingia kwenye sinagogi akaanza kufundisha. 22 Watu wakashangaa sana mafundisho yake, kwa maana aliwafundisha kama yeye aliye na mamlaka, wala si kama walimu wa sheria. 23 Wakati huo huo, palikuwa na mtu kwenye sinagogi lao aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu, 24 naye alikuwa akipiga kelele akisema, “Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Je, umekuja kutuangamiza? Nakujua wewe ni nani, wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu!”

25 Lakini Yesu akamkemea, akamwambia, “Nyamaza kimya! Nawe umtoke!” 26 Yule pepo mchafu akamtikisatikisa sana huyo mtu kwa nguvu akipiga kelele kwa sauti kubwa, kisha akamtoka.

27 Watu wote wakashangaa, hata kuulizana wao kwa wao, “Haya ni mambo gani? Ni mafundisho mapya, tena yenye mamlaka! Anaamuru hata pepo wachafu nao wanamtii!” 28 Sifa zake zikaanza kuenea kwa upesi katika eneo lote la karibu na Galilaya.

Yesu Amponya Mama Mkwe Wa Simoni

29 Mara walipotoka katika sinagogi, walikwenda pamoja na Yakobo na Yohana hadi nyumbani kwa Simoni na Andrea. 30 Mama mkwe wa Simoni alikuwa kitandani, ana homa, nao wakamweleza Yesu habari zake. 31 Hivyo Yesu akamwendea, akamshika mkono na kumwinua. Kisha homa ikamwacha, naye akaanza kuwahudumia.

Yesu Aponya Wengi

32 Jioni ile baada ya jua kutua, watu wakamletea Yesu wagonjwa wote na waliopagawa na pepo wachafu. 33 Mji wote ukakusanyika mbele ya nyumba hiyo. 34 Yesu akawaponya watu wengi waliokuwa na magonjwa ya aina mbalimbali. Akawatoa pepo wachafu wengi, lakini hakuwaacha hao pepo wachafu waseme kwa sababu walimjua kuwa yeye ni nani.

Yesu Aondoka Kapernaumu Na Kwenda Galilaya

35 Mapema sana alfajiri kulipokuwa bado kungali giza, Yesu akaamka, akaondoka, akaenda mahali pa faragha, ili kuomba. 36 Simoni na wenzake wakaenda kumtafuta, 37 nao walipomwona, wakamwambia, “Kila mtu anakutafuta!”

38 Yesu akawajibu, “Twendeni mahali pengine kwenye vijiji vya jirani, ili niweze kuhubiri huko nako, kwa sababu hicho ndicho nilichokuja kukifanya.” 39 Kwa hiyo akazunguka Galilaya kote, akihubiri katika masinagogi yao na kutoa pepo wachafu.

Yesu Amtakasa Mwenye Ukoma

40 Mtu mmoja mwenye ukoma alimjia Yesu, akamwomba akipiga magoti, akamwambia, “Ukitaka, waweza kunitakasa.”

41 Yesu akiwa amejawa na huruma, akanyosha mkono wake akamgusa, akamwambia, “Nataka takasika!” 42 Mara ukoma ukamtoka, naye akatakasika. 43 Baada ya Yesu kumwonya vikali, akamruhusu aende zake 44 akimwambia, “Hakikisha humwambii mtu ye yote habari hizi, bali nenda ukajionyeshe kwa kuhani na ukatoe sadaka kwa ajili ya kutakasika kwako kama alivyoamuru Mose kuwa ushuhuda kwao.” 45 Lakini yule mtu akaenda akaanza kutangaza habari za kuponywa kwake waziwazi. Kwa hiyo Yesu hakuweza tena kuingia katika miji waziwazi isipokuwa alikaa sehemu zisizo na watu. Lakini bado watu wakamfuata huko kutoka kila upande.

Copyright information for Neno