Mark 14

Shauri La Kumwua Yesu

Zilikuwa zimebaki siku mbili tu kabla ya Sikukuu ya Pasaka na Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu. Viongozi wa makuhani na walimu wa sheria walikuwa wakitafuta njia ya kumkamata Yesu kwa hila na kumwua, kwa kuwa walisema, “Tusilifanye jambo hili wakati wa Sikukuu, maana watu wanaweza wakafanya ghasia.”

Yesu Kupakwa Mafuta Huko Bethania

Yesu alipokuwa huko Bethania nyumbani kwa Simoni aliyekuwa na ukoma, wakati alipokuwa ameketi mezani akila chakula cha jioni, mwanamke mmoja aliingia akiwa na chupa ya marhamu yenye manukato ya nardo
14.3 Nardo ni aina ya manukato yaliyotengenezwa kutokana na mimea yenye mizizi inayotoa harufu nzuri
safi ya thamani kubwa. Akaivunja hiyo chupa, akamiminia hayo manukato kichwani mwa Yesu.

Baadhi ya watu waliokuwapo pale walikuwa wakisemezana wao kwa wao, “Kwa nini ubadhirifu huu wa manukato? Mafuta haya yangeweza kuuzwa kwa zaidi ya dinari
14.5 Dinari 300 ni sawa na mshahara wa kibarua wa siku 300
300 na fedha hizo wakapewa maskini.” Wakamkemea vikali huyo mwanamke.

Lakini Yesu akawaambia, “Kwa nini mnamsumbua? Mwacheni! Amenitendea jambo la kupendeza. Maskini mnao pamoja nanyi siku zote na mnaweza kuwasaidia wakati wo wote mnaotaka. Lakini mimi hamko nami daima. Huyu mwanamke amenitendea lile aliloweza. Ameutia mwili wangu manukato kuniandaa kwa maziko yangu. Amin, amin nawaambia, mahali po pote duniani ambapo Injili itahubiriwa, jambo hili alilotenda huyu mwanamke litatajwa kwa ukumbusho wake.”

Yuda Akubali Kumsaliti Yesu

10 Kisha Yuda Iskariote, mmoja wa wale wanafunzi kumi na wawili wa Bwana Yesu, akaenda kwa viongozi wa makuhani ili kumsaliti Yesu kwao. 11 Walifurahi sana kusikia jambo hili na wakaahidi kumpa fedha. Hivyo yeye akawa anatafuta wasaa mzuri wa kumtia Yesu mikononi mwao.

Yesu Ala Pasaka Na Wanafunzi Wake

12 Siku ya kwanza ya Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, siku ambayo kwa desturi kondoo wa Pasaka huchinjwa, wanafunzi wa Yesu wakamwuliza, “Unataka tuende wapi ili tukuandalie mahali pa kula Pasaka?”

13 Basi akawatuma wawili miongoni mwa wanafunzi wake, akawaambia, “Nendeni mjini, huko mtakutana na mwanaume amebeba mtungi wa maji. Mfuateni. 14 Mwambieni mwenye nyumba ile atakayoingia, ‘Mwalimu anauliza, kiko wapi chumba changu kwa ajili ya wageni ambamo nitakula Pasaka pamoja na wanafunzi wangu?’ 15 Atawaonyesha chumba kikubwa ghorofani, kilichopambwa tena kilicho tayari. Tuandalieni humo.”

16 Wale wanafunzi wakaondoka na kwenda mjini, nao wakakuta kila kitu kama alivyowaambia. Hivyo wakaandaa chakula cha Pasaka.

17 Ilipofika jioni, Yesu akaja pamoja na wale wanafunzi wake kumi na wawili. 18 Walipokwisha kuketi kwenye nafasi zao, wakati wakila Yesu akawaambia, “Amin, nawaambia, mmoja wenu atanisaliti, yaani, yeye anayekula pamoja nami.”

19 Wakaanza kuhuzunika na kumwambia mmoja baada ya mwingine, “Je, ni mimi Bwana?”

20 Akawajibu, “Ni mmoja miongoni mwenu ninyi kumi na wawili, yule anayechovya mkate kwenye bakuli pamoja nami. 21 Kwa kuwa Mwana wa Adamu yu aenda zake kama vile alivyoandikiwa. Lakini ole wake mtu yule amsalitiye Mwana wa Adamu! Ingelikuwa heri kama mtu huyo asingelizaliwa.”

Kuanzishwa Kwa Meza Ya Bwana

22 Walipokuwa wakila, Yesu akachukua mkate, akashukuru, akaumega na kuwapa wanafunzi wake akisema, “Twaeni mle, huu ndio mwili wangu.”

23 Kisha akachukua kikombe, akashukuru, akawapa wanafunzi wake, wote wakanywa kutoka humo.

24 Akawaambia, “Hii ndiyo damu yangu ya Agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi. 25 Amin nawaambia, sitakunywa tena uzao wa mzabibu mpaka siku ile nitakapokunywa mpya katika Ufalme wa Mungu.”

26 Walipokwisha kuimba wimbo, wakatoka wakaenda kwenye Mlima wa Mizeituni.

Yesu Atabiri Kuwa Petro Atamkana

27 Yesu akawaambia, “Ninyi nyote mtaniacha, kwa maana imeandikwa: “ ‘Nitampiga mchungaji,
nao kondoo watatawanyika.’


28 Lakini baada ya kufufuka, nitawatangulia kwenda Galilaya.”

29 Petro akasema, “Hata kama wengine wote watakuacha, mimi sitakuacha.”

30 Yesu akamwambia, “Amin, nakuambia; leo, usiku huu, kabla jogoo hajawika mara mbili, utanikana mara tatu.”

31 Lakini Petro akasisitiza akasema, “Hata kama inanipasa kufa pamoja nawe, sitakukana.” Nao wale wanafunzi wengine wote wakasema vivyo hivyo.

Yesu Akiomba Bustanini Gethsemane

32 Wakaenda mahali paitwapo Gethsemane, Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kaeni hapa wakati ninakwenda kule kuomba.” 33 Kisha akawachukua pamoja naye Petro, Yakobo na Yohana. Naye akaanza kuhuzunika sana na kutaabika. 34 Akawaambia, “Moyo wangu umejawa na huzuni kiasi cha kufa. Kaeni hapa na mkeshe.”

35 Akaenda mbele kidogo, akajitupa chini kifudifudi akaomba akisema, kama ikiwezekana saa hiyo ya mateso imwepuke. 36 Akasema, “Abba
14.36 Abba ni neno la Kiaramu ambalo maana yake ni Baba; ni mtoto wa kuzaa tu angeweza kulitumia kwa baba yake
, Baba, mambo yote yawezekana kwako. Niondolee kikombe hiki, lakini si kama nitakavyo mimi, bali mapenzi yako yatimizwe.”

37 Akarudi kwa wanafunzi wake akawakuta wamelala, naye akamwambia Petro, “Simoni, umelala? Je, hukuweza kukesha hata kwa saa moja? 38 Kesheni na kuomba msije mkaingia majaribuni. Roho iko radhi lakini mwili ni dhaifu.”

39 Akaenda tena kuomba akisema maneno yale yale. 40 Aliporudi kwa wanafunzi wake, akawakuta tena wamelala, kwa sababu macho yao yalikuwa mazito. Nao hawakujua la kumwambia.

41 Akaja mara ya tatu, akawaambia, “Bado mmelala na kupumzika? Imetosha! Saa imewadia. Tazama, Mwana wa Adamu anasalitiwa mikononi mwa wenye dhambi. 42 Amkeni! Twendeni zetu! Tazameni, msaliti wangu yuaja!”

Yesu Akamatwa

43 Yesu alipokuwa bado anazungumza, Yuda, mmoja wa wale wanafunzi kumi na wawili, akatokea akiwa pamoja na umati wa watu wenye panga na marungu, waliokuwa wametumwa na viongozi wa makuhani, walimu wa sheria na wazee.

44 Basi Yuda, yule msaliti, alikuwa amewapa ishara wale watu kuwa: “Yule nitakayembusu, ndiye, mkamateni na mchukueni akiwa chini ya ulinzi.” 45 Kwa hiyo Yuda alipofika, akamwendea Yesu akamwambia, “Rabi”
14.45 Rabi ni neno la Kiebrania ambalo maana yake ni daktari, mwalimu au bwana. Walikuwa na madaraja matatu: La chini kabisa rab (bwana), la pili rabi (bwana wangu), na la juu kabisa raboni (mkuu wangu, bwana wangu mkuu)
na kumbusu.
46 Wale watu wakamkamata Yesu, wakamweka chini ya ulinzi. 47 Ndipo mmoja wa wale waliokuwa wamesimama karibu akachomoa upanga wake na kumpiga mtumishi wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio.

48 Kisha Yesu akawaambia, “Mmekuja mkiwa na panga na marungu kana kwamba mimi ni mnyang'anyi? 49 Siku zote nilikuwa pamoja nanyi nikifundisha Hekaluni, wala hamkunikamata. Lakini maandiko na yatimie.” 50 Ndipo wanafunzi wake wote wakamwacha, wakakimbia.

51 Kijana mmoja, ambaye hakuwa amevaa kitu isipokuwa alijitanda nguo ya kitani, alikuwa akimfuata Yesu. Wakamkamata, 52 akakimbia uchi, akaliacha vazi lake.

Yesu Mbele Ya Baraza

53 Wakampeleka Yesu kwa Kuhani Mkuu, nao viongozi wa makuhani, wazee na walimu wa sheria wakakusanyika pamoja. 54 Petro akamfuata kwa mbali, mpaka kwenye ua wa Kuhani Mkuu. Huko akaketi pamoja na walinzi, akiota moto.

55 Viongozi wa makuhani na wajumbe wote wa Baraza
14.55 Baraza hapa ina maana ya Sanhedrin ambalo lilikuwa ndilo Baraza la juu kabisa la utawala wa Kiyahudi, lililoundwa na wazee 70 pamoja na Kuhani Mkuu
walikuwa wanatafuta ushahidi dhidi ya Yesu ili wapate kumwua, lakini hawakupata.
56 Wengi wakatoa ushahidi wa uongo dhidi yake, lakini maelezo yao hayakukubaliana.

57 Ndipo wengine wakasimama wakatoa ushahidi wa uongo dhidi yake, wakisema, 58 “Sisi tulimsikia akisema, ‘Mimi nitalibomoa Hekalu hili lililojengwa na wanadamu na katika siku tatu nitajenga jingine ambalo halikujengwa na wanadamu.’ ” 59 Lakini hata hivyo, ushahidi wao haukukubaliana.

60 Kuhani Mkuu akasimama mbele ya hilo Baraza akamwuliza Yesu, “Je, wewe huwezi kujibu mashtaka haya ambayo watu hawa wameleta juu yako?” 61 Lakini Yesu akakaa kimya, hakusema neno lo lote.

Kuhani Mkuu akamwuliza tena, “Je, wewe ndiwe Kristo
14:61 Yaani Masiya
, Mwana wa Mungu Mbarikiwa?”

62 Yesu akajibu, “Mimi ndimi, nanyi mtamwona Mwana wa Adamu ameketi mkono wa kuume wa Mwenye Nguvu, akija na mawingu ya mbinguni.”

63 Kuhani Mkuu akararua mavazi yake, akasema, “Tuna haja gani tena ya mashahidi zaidi? 64 Ninyi mmesikia hayo makufuru. Uamuzi wenu ni nini?”

Wote wakamhukumu kwamba anastahili kifo.
65 Kisha baadhi ya watu wakaanza kumtemea mate, wakamfunga kitambaa machoni, wakampiga kwa ngumi na kumwambia, “Tabiri ni nani aliyekupiga!” Walinzi wakamchukua na kumpiga makofi.

Petro Amkana Yesu

66 Petro alipokuwa bado yuko chini kwenye ua wa jumba la kifalme, tazama akaja mmoja wa watumishi wa kike wa Kuhani Mkuu. 67 Alipomwona Petro akiota moto, akamtazama sana, akamwambia,

“Wewe pia ulikuwa pamoja na Yesu, Mnazareti.”

68 Lakini Petro akakana, akasema, “Sijui wala sielewi unalosema.” Naye akaondoka kuelekea kwenye njia ya kuingilia.

69 Yule mtumishi wa kike alipomwona hapo mahali, akawaambia tena wale waliokuwa wamesimama hapo, “Huyu mtu ni mmoja wao.” 70 Lakini Petro akakana tena.

Baada ya muda kidogo wale waliokuwa wamesimama hapo karibu na Petro wakamwambia, “Hakika wewe ni mmoja wao, kwa maana wewe pia ni Mgalilaya!”
71 Petro akaanza kulaani na kuapa, akawaambia, “Simjui huyu mtu mnayesema habari zake.”

72 Papo hapo jogoo akawika mara ya pili. Ndipo Petro akakumbuka lile neno Yesu alilokuwa amemwambia, “Kabla jogoo hajawika mara mbili, utanikana mara tatu.” Akavunjika moyo, akalia sana.

Copyright information for Neno