Mark 15

Yesu Mbele Ya Pilato

Asubuhi na mapema, viongozi wa makuhani, pamoja na wazee, walimu wa sheria na Baraza lote, wakafikia uamuzi. Wakamfunga Yesu, wakamchukua na kumkabidhi kwa Pilato.

Pilato akamwuliza, “Je, wewe ndiye Mfalme wa Wayahudi?”

Yesu akajibu, “Wewe umesema.”

Viongozi wa makuhani wakamshtaki kwa mambo mengi. Pilato akamwuliza tena, “Je, huna la kujibu? Tazama ni mashtaka mangapi wanayaleta juu yako.”

Lakini Yesu hakuendelea kujibu, hivyo Pilato akashangaa.

Pilato Amtoa Yesu Ili Akasulibiwe

Ilikuwa desturi wakati wa Sikukuu ya Pasaka kumfungulia mfungwa ye yote ambaye watu wangemtaka. Wakati huo, mtu mmoja aitwaye Baraba alikuwa amefungwa gerezani pamoja na waasi wengine waliokuwa wamesababisha mauaji wakati wa maasi yaliyotokea dhidi ya serikali. Ule umati wa watu ukamjia Pilato na kumwomba awafanyie kama ilivyokuwa desturi yake.

Pilato akawauliza, “Mnataka niwafungulie huyu Mfalme wa Wayahudi?” 10 Kwa maana yeye alitambua kuwa viongozi wa makuhani walikuwa wamemtia Yesu mikononi mwake kwa ajili ya wivu. 11 Lakini viongozi wa makuhani wakauchochea ule umati wa watu wamwombe awafungulie Baraba badala yake.

12 Pilato akawauliza tena, “Basi mnataka nifanye nini na huyu mtu mnayemwita Mfalme wa Wayahudi?”

13 Wakapiga kelele wakisema, “Msulibishe!”

14 Akawauliza, “Kwa nini? Amefanya kosa gani?”

Lakini wao wakapiga kelele kwa nguvu zaidi, wakisema, “Msulibishe!”

15 Pilato akitaka kuuridhisha ule umati wa watu, akawafungulia Baraba, naye baada ya kuamuru Yesu achapwe mijeledi, akamtoa ili asulibishwe.

Maaskari Wamdhihaki Yesu

16 Askari wakampeleka Yesu hadi kwenye ukumbi wa ndani wa jumba la kifalme, ndio Praitorio
15.16 Praitorio maana yake ni makao makuu ya mtawala; ni jumba la kifalme lililokuwa linakaliwa na Pontio Pilato huko Yerusalemu, palipokuwa na kiti cha hukumu
, wakakusanya kikosi kizima cha Askari.
17 Wakamvalisha Yesu joho la zambarau, wakasokota taji ya miiba, wakamvisha kichwani. 18 Wakaanza kumsalimu kwa dhihaka, “Salamu, Mfalme wa Wayahudi!” 19 Wakampiga kwa fimbo ya mwanzi tena na tena kichwani na kumtemea mate. Wakapiga magoti mbele yake wakamsujudia kwa kumdhihaki. 20 Walipokwisha kumdhihaki, wakamvua lile joho la zambarau, wakamvika zile nguo zake mwenyewe. Kisha wakamtoa nje ili wakamsulibishe.

Kusulibiwa Kwa Yesu

21 Mtu mmoja kutoka Kirene, jina lake Simoni, baba yao Aleksanda na Rufo, alikuwa anapita zake kuingia mjini kutoka shamba, wakamlazimisha aubebe ule msalaba wa Yesu. 22 Kisha wakampeleka Yesu mpaka mahali palipoitwa Golgotha (ambayo, maana yake ni Mahali pa Fuvu la Kichwa). 23 Nao wakampa divai iliyochanganywa na manemane, lakini hakuinywa. 24 Basi wakamsulibisha, nazo nguo zake wakagawana miongoni mwao kwa kuzipigia kura ili kuamua ni nini kila mtu atakachochukua.

25 Ilikuwa yapata saa tatu asubuhi walipomsulibisha. 26 Tangazo likaandikwa la mashtaka dhidi yake lenye maneno haya: “MFALME WA WAYAHUDI.” 27 Pamoja naye walisulibiwa wanyang'anyi wawili, mmoja upande wake wa kuume na mwingine upande wa kushoto. 28 Nayo maandiko yakatimizwa, yale yasemayo, “Alihesabiwa pamoja na watenda dhambi.” 29 Watu waliokuwa wakipita karibu wakamtukana na kutikisa vichwa vyao kwa mzaha wakisema, “Aha! Wewe ambaye ungelibomoa Hekalu na kulijenga kwa siku tatu, 30 basi ujiokoe mwenyewe na ushuke kutoka msalabani.”

31 Vivyo hivyo viongozi wa makuhani pamoja na walimu wa sheria wakamdhihaki miongoni mwao wakisema, “Yeye aliwaokoa wengine, lakini hawezi kujiokoa mwenyewe! 32 Basi huyu Kristo
15:32 Yaani Masiya
, huyu Mfalme wa Wayahudi, ashuke sasa kutoka msalabani, ili tupate kuona na kuamini.” Wale waliosulibiwa pamoja naye pia wakamtukana.

Kifo Cha Yesu Msalabani

33 Ilipofika saa sita, giza lilifunika nchi yote mpaka saa tisa. 34 Mnamo saa tisa Yesu akalia kwa sauti kuu, akasema, “Eloi, Eloi lama Sabakthani?” Maana yake, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?”

35 Baadhi ya watu waliokuwa wamesimama karibu waliposikia maneno hayo, wakasema, “Msikieni anamwita Eliya.”

36 Mtu mmoja akaenda mbio, akachovya sifongo kwenye siki, akaiweka kwenye mwanzi, akampa Yesu ili anywe akisema, “Basi mwacheni, hebu tuone kama Eliya atakuja kumshusha kutoka hapo msalabani.”

37 Kisha Yesu akatoa sauti kuu, akakata roho.

38 Pazia la Hekalu likachanika vipande viwili kuanzia juu hadi chini. 39 Basi yule jemadari, aliyekuwa amesimama hapo mbele ya msalaba wa Yesu, aliposikia ile sauti yake na kuona jinsi alivyokata roho, akasema, “Hakika mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu!”

40 Walikuwapo pia wanawake waliokuwa wakiangalia kwa mbali, ambao miongoni mwao alikuwa Maria Magdalene, Maria mama yao Yakobo mdogo na Yose, pia na Salome. 41 Hawa walifuatana na Yesu na kumhudumia alipokuwa Galilaya. Pia walikuwapo wanawake wengine wengi waliokuwa wamekuja pamoja naye Yerusalemu.

Maziko Ya Yesu

42 Ilipofika jioni, kwa kuwa ilikuwa Siku ya Maandalizo, siku moja kabla ya Sabato, 43 Yosefu wa Arimathaya mtu aliyeheshimiwa katika Baraza, ambaye yeye mwenyewe alikuwa anautarajia Ufalme wa Mungu, akamwendea Pilato kwa ujasiri na kumwomba huo mwili wa Yesu. 44 Pilato alikuwa akijiuliza kama Yesu alikuwa amekwisha kufa. Akamwita yule jemadari, akamwuliza iwapo Yesu alikuwa amekwisha kufa. 45 Baada ya kupata habari kutoka kwa yule jemadari kwamba kweli amekwisha kufa, Pilato akampa Yosefu ruhusa ya kuuchukua huo mwili. 46 Hivyo Yosefu akanunua kitambaa cha kitani safi, akaushusha mwili wa Yesu kutoka msalabani, akauviringishia kile kitambaa cha kitani na akamweka ndani ya kaburi lililochongwa kwenye mwamba. Kisha akalivingirisha jiwe kwenye ingilio la kaburi. 47 Maria Magdalene na Maria mamaye Yose walipaona mahali pale alipolazwa.

Copyright information for Neno