Mark 1

Mahubiri Ya Yohana Mbatizaji

1Mwanzo wa Injili ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu.

2Kama ilivyoandikwa katika kitabu cha nabii Isaya: “Tazama, namtuma mjumbe wangu mbele yako,
yeye atakayeitengeneza njia yako”:
3“sauti ya mtu aliaye nyikani.
‘Itengenezeni njia ya Bwana,
yanyosheni mapito yake.’ ”


4Yohana alikuja, akibatiza huko nyikani, akihubiri ubatizo wa toba kwa ajili ya ondoleo la dhambi. 5Watu kutoka Uyahudi wote na sehemu zote za Yerusalemu walikuwa wakimwendea, naye akawabatiza katika Mto Yordani, wakitubu dhambi zao. 6Yohana alivaa mavazi yaliyotengenezwa kwa singa za ngamia na mkanda wa ngozi kiunoni mwake. Chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwitu. 7Naye alihubiri akisema, “Baada yangu atakuja yeye aliye na uwezo kuliko mimi, ambaye sistahili hata kuinama na kulegeza kamba za viatu vyake. 8Mimi nawabatiza kwa maji, lakini yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu.”

Ubatizo Wa Yesu

9Wakati huo Yesu akaja kutoka Nazareti ya Galilaya, naye akabatizwa na Yohana katika Mto Yordani. 10Yesu alipokuwa akitoka ndani ya maji, aliona mbingu zikifunguka na Roho akishuka juu yake kama hua. 11Nayo sauti kutoka mbinguni ikasema, “Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu, ambaye nimependezwa nawe.”

Majaribu Ya Yesu

12Wakati huo huo, Roho akamwongoza Yesu kwenda nyikani, 13naye akawa huko nyikani kwa muda wa siku arobaini, akijaribiwa na Shetani. Alikaa na wanyama wa mwituni, nao malaika wakamhudumia.

Yesu Aanza Kuhubiri

14Baada ya Yohana kukamatwa na kutiwa gerezani, Yesu aliingia Galilaya akaanza kuhubiri habari njema ya Mungu, 15akisema, “Wakati umewadia, Ufalme wa Mungu umekaribia. Tubuni na kuiamini Habari Njema.”

Yesu Awaita Wanafunzi Wanne

16Yesu alipokuwa akitembea kandokando ya Bahari ya Galilaya alimwona Simoni na Andrea nduguye wakizitupa nyavu zao baharini, kwa kuwa hawa wawili walikuwa wavuvi. 17Yesu akawaambia, “Njoni nifuateni, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu.” 18Mara wakaacha nyavu zao, wakamfuata Yesu.

19Alipokwenda mbele kidogo, akamwona Yakobo mwana wa Zebedayo na Yohana nduguye, wakiwa kwenye mashua yao wakizitengeneza nyavu zao. 20Papo hapo akawaita, nao wakamwacha Zebedayo baba yao kwenye mashua pamoja na watumishi wa kuajiriwa, nao wakamfuata Yesu.

Yesu Amtoa Pepo Mchafu

21Wakaenda mpaka Kapernaumu. Ilipofika siku ya Sabato, mara Yesu akaingia kwenye sinagogi akaanza kufundisha. 22Watu wakashangaa sana mafundisho yake, kwa maana aliwafundisha kama yeye aliye na mamlaka, wala si kama walimu wa sheria. 23Wakati huo huo, palikuwa na mtu kwenye sinagogi lao aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu, 24naye alikuwa akipiga kelele akisema, “Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Je, umekuja kutuangamiza? Nakujua wewe ni nani, wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu!”

25Lakini Yesu akamkemea, akamwambia, “Nyamaza kimya! Nawe umtoke!” 26Yule pepo mchafu akamtikisatikisa sana huyo mtu kwa nguvu akipiga kelele kwa sauti kubwa, kisha akamtoka.

27Watu wote wakashangaa, hata kuulizana wao kwa wao, “Haya ni mambo gani? Ni mafundisho mapya, tena yenye mamlaka! Anaamuru hata pepo wachafu nao wanamtii!” 28Sifa zake zikaanza kuenea kwa upesi katika eneo lote la karibu na Galilaya.

Yesu Amponya Mama Mkwe Wa Simoni

29Mara walipotoka katika sinagogi, walikwenda pamoja na Yakobo na Yohana hadi nyumbani kwa Simoni na Andrea. 30Mama mkwe wa Simoni alikuwa kitandani, ana homa, nao wakamweleza Yesu habari zake. 31Hivyo Yesu akamwendea, akamshika mkono na kumwinua. Kisha homa ikamwacha, naye akaanza kuwahudumia.

Yesu Aponya Wengi

32Jioni ile baada ya jua kutua, watu wakamletea Yesu wagonjwa wote na waliopagawa na pepo wachafu. 33Mji wote ukakusanyika mbele ya nyumba hiyo. 34Yesu akawaponya watu wengi waliokuwa na magonjwa ya aina mbalimbali. Akawatoa pepo wachafu wengi, lakini hakuwaacha hao pepo wachafu waseme kwa sababu walimjua kuwa yeye ni nani.

Yesu Aondoka Kapernaumu Na Kwenda Galilaya

35Mapema sana alfajiri kulipokuwa bado kungali giza, Yesu akaamka, akaondoka, akaenda mahali pa faragha, ili kuomba. 36Simoni na wenzake wakaenda kumtafuta, 37nao walipomwona, wakamwambia, “Kila mtu anakutafuta!”

38Yesu akawajibu, “Twendeni mahali pengine kwenye vijiji vya jirani, ili niweze kuhubiri huko nako, kwa sababu hicho ndicho nilichokuja kukifanya.” 39Kwa hiyo akazunguka Galilaya kote, akihubiri katika masinagogi yao na kutoa pepo wachafu.

Yesu Amtakasa Mwenye Ukoma

40Mtu mmoja mwenye ukoma alimjia Yesu, akamwomba akipiga magoti, akamwambia, “Ukitaka, waweza kunitakasa.”

41Yesu akiwa amejawa na huruma, akanyosha mkono wake akamgusa, akamwambia, “Nataka takasika!” 42Mara ukoma ukamtoka, naye akatakasika. 43Baada ya Yesu kumwonya vikali, akamruhusu aende zake 44akimwambia, “Hakikisha humwambii mtu ye yote habari hizi, bali nenda ukajionyeshe kwa kuhani na ukatoe sadaka kwa ajili ya kutakasika kwako kama alivyoamuru Mose kuwa ushuhuda kwao.” 45Lakini yule mtu akaenda akaanza kutangaza habari za kuponywa kwake waziwazi. Kwa hiyo Yesu hakuweza tena kuingia katika miji waziwazi isipokuwa alikaa sehemu zisizo na watu. Lakini bado watu wakamfuata huko kutoka kila upande.

Copyright information for Neno