Matthew 15

Mapokeo Ya Wazee

1Ndipo baadhi ya Mafarisayo na walimu wa sheria wakamjia Yesu kutoka Yerusalemu na kumwuliza, 2“Mbona wanafunzi wako wanakiuka mapokeo ya wazee waliopita? Kwa maana wao hawanawi mikono yao kabla ya kula!”

3Yesu akawajibu, “Mbona ninyi mnavunja amri ya Mungu kwa ajili ya mapokeo yenu? 4Kwa maana Mungu alisema, ‘Waheshimu baba yako na mama yako’ na ‘Ye yote amtukanaye baba yake au mama yake, na auawe.’ 5Lakini ninyi mwafundisha kwamba mtu akimwambia baba yake au mama yake, ‘Kile ambacho ningeweza kukusaidia kimewekwa wakfu kwa Mungu,’ basi hana tena sababu ya kumsaidia baba yake. 6Basi kwa ajili ya mafundisho yenu mnavunja amri ya Mungu. 7Ninyi wanafiki! Isaya alikuwa sawa alipotabiri juu yenu kwamba: 8“ ‘Watu hawa huniheshimu kwa midomo yao,
lakini mioyo yao iko mbali nami.
9Kuniabudu kwao ni bure,
nayo mafundisho yao
ni maagizo ya wanadamu tu.’ ”


Vitu Vitiavyo Unajisi

10Yesu akaita ule umati wa watu akawaambia, “Sikilizeni na muelewe: 11kinachomfanya mtu kuwa najisi mbele za Mungu si kile kiingiacho kinywani mwake, bali ni kile kitokacho kinywani mwake.”

12Kisha wanafunzi wake wakamjia na kumwuliza, “Je, unajua kwamba Mafarisayo walichukizwa sana waliposikia yale uliyosema?”

13Akawajibu, “Kila pando ambalo Baba yangu wa mbinguni hakulipanda, litang'olewa. 14Waacheni, wao ni viongozi vipofu, wanaoongoza vipofu. Kama kipofu akimwongoza kipofu mwenzake, wote wawili watatumbukia shimoni.”

15Petro akasema, “Tuelezee maana ya huu mfano.”

16Yesu akawauliza, “Je, bado ninyi hamfahamu? 17Je, hamuelewi kwamba cho chote kiingiacho kinywani huenda tumboni na hatimaye hutolewa nje kikiwa uchafu? 18Lakini kitokacho kinywani hutoka moyoni, na hiki ndicho kimtiacho mtu unajisi. 19Kwa maana ndani ya moyo hutoka mawazo mabaya, uuaji, uzinzi, uasherati, wizi, ushahidi wa uongo na masingizio. 20Haya ndiyo yamtiayo mtu unajisi, lakini kula bila kunawa mikono hakumtii mtu unajisi.”

Imani Ya Mwanamke Mkanaani

21Yesu aliondoka mahali pale akaenda sehemu za Tiro na Sidoni. 22Mwanamke mmoja Mkanaani aliyeishi jirani na sehemu hizo akaja kwake, akilia, akasema, “Nihurumie, Ee Bwana, Mwana wa Daudi, binti yangu amepagawa na pepo mchafu na anateseka sana.”

23Lakini Yesu hakumjibu neno. Hivyo wanafunzi wake wakamwendea na kumsihi sana, wakisema, “Mwambie aende zake, kwa maana anaendelea kutupigia kelele.”

24Yesu akajibu, “Nimetumwa tu kwa ajili ya kondoo wa Israeli waliopotea.”

25Lakini yule mwanamke akaja, akapiga magoti mbele ya Yesu, akasema, “Bwana, nisaidie!”

26Yesu akajibu, “Si haki kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.”

27Yule mwanamke akajibu, “Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa hula makombo yanayoanguka kutoka kwenye meza za bwana zao.”

28Ndipo Yesu akamwambia, “Mwanamke, imani yako ni kubwa! Iwe kwako kama unavyotaka.” Naye binti yake akapona tangu saa ile.

Yesu Aponya Watu Wengi

29Yesu akaondoka na kwenda kando ya Bahari ya Galilaya. Kisha akapanda mlimani, akaketi huko. 30Umati mkubwa wa watu ukamjia, wakiwaleta vilema, vipofu, viwete, bubu na wengine wengi, wakawaweka miguuni pake, naye akawaponya. 31Hao watu wakashangaa walipoona bubu wakisema, vilema wakipona, viwete wakitembea na vipofu wakiona, wakamtukuza Mungu wa Israeli.

Yesu Alisha Watu Elfu Nne

32Kisha Yesu akawaita wanafunzi wake akawaambia, “Ninahurumia huu umati wa watu, kwa sababu sasa wamekuwa pamoja nami kwa muda wa siku tatu na hawana chakula cho chote, nami sipendi kuwaaga wakiwa na njaa wasije wakazimia njiani.”

33Wanafunzi wake wakasema, “Tutapata wapi mikate ya kutosha kuwalisha umati huu wa watu mkubwa namna hii, nasi tuko nyikani?”

34Yesu akawauliza, “Mnayo mikate mingapi?”

Wakamjibu, “Tunayo mikate saba na visamaki vichache.”

35Yesu akawaambia ule umati wa watu waketi chini. 36Kisha akachukua ile mikate saba na wale samaki, naye akiisha kumshukuru Mungu, akavimega na kuwapa wanafunzi wake, nao wakawapa ule umati wa watu. 37Wote wakala na kushiba. Baadaye wanafunzi wakakusanya vipande vilivyosalia, wakajaza vikapu saba. 38Idadi ya watu walikuwa wanaume 4,000, bila kuhesabu wanawake na watoto. 39Baada ya kuaga ule umati wa watu, Yesu aliingia chomboni akaenda sehemu za Magadani
15.39 Magadani ni Magdala, mji wa Galilaya, kama kilomita 16 kusini mwa Kapernaumu
.

Copyright information for Neno