Matthew 21

Yesu Anaingia Yerusalemu Kwa Shangwe

Walipokuwa wanakaribia Yerusalemu, wakafika Bethfage katika Mlima wa Mizeituni, ndipo Yesu akawatuma wanafunzi wake wawili, akiwaambia, “Ingieni katika kijiji kilichoko mbele yenu, nanyi mtakuta punda amefungwa na mwana-punda pamoja naye. Wafungueni na mniletee. Kama mtu ye yote akiwasemesha lo lote, mwambieni kwamba Bwana ana haja nao, naye atawaruhusu mwalete mara.”

Haya yalitukia ili litimie lile lililonenwa na nabii, akisema: “Mwambieni Binti Sayuni,
‘Tazama, mfalme wako anakuja kwako,
ni mnyenyekevu, naye amepanda punda,
juu ya mwana-punda, mtoto wa punda.’ ”Wale wanafunzi wakaenda, wakafanya kama vile Yesu alivyokuwa amewaagiza. Wakamleta yule punda na mwana-punda, nao wakatandika mavazi yao juu ya hao punda na Yesu akaketi juu yake. Umati mkubwa wa watu wakatandika nguo zao barabarani na wengine wakakata matawi kutoka kwenye miti wakayatandika barabarani. Ule umati wa watu uliomtangulia na ule uliomfuata ukapiga kelele ukisema, “Hosana
21:9 Kiebrania kusema Okoa, basi likawa neno la shangwe
Mwana wa Daudi!”
“Amebarikiwa yeye ajaye kwa Jina la Bwana!”
“Hosana juu mbinguni!”10 Yesu alipoingia Yerusalemu, mji wote ukataharuki, watu wakauliza, “Huyu ni nani?”

11 Ule umati wa watu ukajibu, “Huyu ni Yesu, yule nabii kutoka Nazareti katika Galilaya.”

Yesu Atakasa Hekalu

12 Yesu akaingia katika eneo la Hekalu na kuwafukuza wote waliokuwa wakinunua na kuuza vitu Hekaluni, akazipindua meza za watu waliokuwa wakibadilisha fedha na viti vya wale waliokuwa wakiuza njiwa. 13 Akawaambia, “Imeandikwa, ‘Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala,’ lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang'anyi.”

14 Vipofu na vilema wakamwendea kule Hekaluni, naye akawaponya. 15 Lakini viongozi wa makuhani na walimu wa sheria walipoona mambo ya ajabu aliyofanya na kuwasikia watoto wakishangilia katika eneo la Hekalu wakisema, “Hosana Mwana wa Daudi”, walikasirika.

16 Wakamwuliza Yesu, “Je, unasikia hayo hawa wanayosema?”

Akawajibu, “Naam; kwani hamkusoma, “ ‘Kutoka katika vinywa vya watoto wachanga
na wale wanaonyonya
umeamuru sifa kamili?’ ”17 Akawaacha, akatoka nje ya mji, akaenda hadi Bethania, akalala huko.

Mtini Wanyauka

18 Asubuhi na mapema, Yesu alipokuwa akirudi mjini, alikuwa na njaa. 19 Akauona mtini kando ya barabara, akaukaribia lakini hakupata tunda lo lote ila majani. Ndipo akauambia, “Wewe na usizae matunda tena kamwe!” Papo hapo ule mtini ukanyauka.

20 Wanafunzi wake walipoona jambo hili wakashangaa, wakamwuliza, “Imekuwaje mtini huu kunyauka ghafula?”

21 Yesu akawajibu, “Amin, amin nawaambia, kama mkiwa na imani wala msiwe na shaka, si kwamba mtaweza kufanya tu yale yaliyofanyika kwa huu mtini, bali hata mkiuambia huu mlima, ‘Ng'oka, ukatupwe baharini,’ nalo litafanyika. 22 Lo lote mtakaloomba katika kusali, mkiamini, mtapokea.”

Wahoji Kuhusu Mamlaka Ya Yesu

23 Yesu alipoingia Hekaluni, viongozi wa makuhani na wazee wa watu wakamjia alipokuwa anafundisha na kusema, “Unafanya mambo haya kwa mamlaka gani, naye ni nani aliyekupa mamlaka hayo?”

24 Yesu akawajibu, “Nami nitawauliza swali moja. Kama mkinijibu, mimi nitawaambia ni kwa mamlaka gani ninafanya mambo haya. 25 Ubatizo wa Yohana, ulitoka wapi? Je, ulitoka mbinguni au kwa wanadamu?”

Wakaanza kuhojiana wao kwa wao na kusema, “Tukisema ulitoka mbinguni atatuuliza, ‘Mbona basi hamkumwamini?’
26 Lakini tukisema, ‘Ulitoka kwa wanadamu’, tunawaogopa hawa watu, maana wote wanamtambua Yohana kuwa ni nabii.”

27 Kwa hiyo wakamjibu Yesu, “Sisi hatujui.”

Ndipo akawaambia, “Wala mimi sitawaambia ni kwa mamlaka gani ninatenda mambo haya.”

Mfano Wa Wana Wawili

28 “Lakini mwaonaje? Mtu mmoja alikuwa na wana wawili. Akamwendea yule wa kwanza akamwambia, ‘Mwanangu, nenda ukafanye kazi kwenye shamba la mizabibu leo.’

29 “Yule mwanawe akamjibu ‘Mimi sitakwenda’, baadaye akabadili mawazo yake akaenda.

30 “Kisha yule baba akamwendea yule mwanawe mwingine akamwambia vile vile. Yeye akajibu, ‘Nitakwenda baba,’ lakini hakwenda.

31 “Ni yupi kati yao hao wawili aliyetimiza kile alichotaka baba yake?”

Wakamjibu, “Ni yule wa kwanza.”

Yesu akawaambia, “Amin, amin nawaambia, watoza ushuru na makahaba wanawatangulia kuingia katika Ufalme wa Mungu.
32 Kwa maana Yohana alikuja kwenu kuwaonyesha njia ya haki, lakini hamkumsadiki, lakini watoza ushuru na makahaba wakamsadiki. Nanyi hata mlipoona hayo, baadaye hamkutubu na kumsadiki.”

Mfano Wa Wapangaji Waovu

33 “Sikilizeni mfano mwingine: Kulikuwa na mtu mmoja mwenye shamba ambaye alipanda mizabibu. Akajenga ukuta kulizunguka, akatengeneza shinikizo ndani yake na akajenga mnara wa ulinzi. Kisha akalikodisha hilo shamba la mizabibu kwa wakulima fulani, naye akaondoka akasafiri kwenda nchi nyingine. 34 Wakati wa mavuno ulipokaribia, akawatuma watumishi wake kwa hao wakulima waliopangishwa ili kukusanya matunda yake.

35 “Wale wapangaji wakawakamata wale watumishi, wakampiga mmoja, wakamwua mwingine na yule wa tatu wakampiga mawe. 36 Kisha akawatuma kwao watumishi wengine, wengi kuliko wale wa kwanza, nao wale wapangaji wakawatendea vile vile. 37 Mwisho wa yote, akamtuma mwanawe kwao, akisema, ‘Watamheshimu mwanangu.’

38 “Lakini wale wapangaji walipomwona mwanawe, wakaambiana wao kwa wao, ‘Huyu ndiye mrithi. Njoni na tumwue ili tuchukue urithi wake.’ 39 Hivyo wakamchukua, wakamtupa nje ya shamba la mizabibu, wakamwua.

40 “Kwa hiyo, huyo mwenye shamba, atakapokuja atawafanyia nini hao wakulima?”

41 Wakamjibu, “Kwa huzuni kuu atawaangamiza kabisa hao wadhalimu na kulipangisha shamba lake kwa wakulima wengine ambao watampatia fungu lake la matunda wakati wa mavuno.”

42 Yesu akawaambia, “Je, hamjasoma katika maandiko kwamba: “ ‘Lile jiwe walilolikataa waashi
limekuwa jiwe kuu la pembeni;
Bwana ndiye aliyefanya jambo hili,
nalo ni la ajabu machoni petu’?43 “Kwa hiyo ninawaambia, Ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu na kupewa watu wengine wawezao kuzaa matunda yake. 44 Yeye aangukaye kwenye jiwe hili atavunjika vipande vipande, lakini yule litakayemwangukia atasagika kabisa.”

45 Viongozi wa Makuhani na Mafarisayo waliposikia mifano ya Yesu, walitambua kuwa alikuwa akiwasema wao. 46 Wakatafuta njia ya kumkamata lakini wakaogopa ule umati wa watu kwa kuwa wao walimwona Yesu kuwa ni nabii.

Copyright information for Neno