Matthew 4

Kujaribiwa Kwa Yesu

1Kisha Yesu akaongozwa na Roho Mtakatifu kuingia nyikani ili akajaribiwe na ibilisi. 2Baada ya kufunga siku arobaini mchana na usiku, hatimaye akaona njaa. 3Mjaribu akamjia na kumwambia, “Kama wewe ndiye Mwana wa Mungu, amuru mawe haya yawe mikate.”

4Lakini Yesu akajibu, “Imeandikwa, ‘Mtu haishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.’ ”

5Ndipo ibilisi akamchukua Yesu mpaka mji mtakatifu wa Yerusalemu na kumweka juu ya mnara mrefu mwembamba wa Hekalu, 6akamwambia, “Kama wewe ndiye Mwana wa Mungu jitupe chini, kwa kuwa imeandikwa, “ ‘Atakuagizia malaika zake,
nao watakuchukua mikononi mwao
ili usije ukajikwaa mguu wako kwenye jiwe.’ ”7Yesu akamjibu, “Pia imeandikwa: ‘Usimjaribu Bwana Mungu wako.’ ”

8Kwa mara nyingine, ibilisi akamchukua Yesu mpaka kwenye kilele cha mlima mrefu na kumwonyesha falme zote za dunia na fahari zake, 9kisha akamwambia, “Nitakupa hivi vyote kama ukinisujudia na kuniabudu.”

10Yesu akamwambia, “Ondoka mbele yangu, Shetani! Kwa maana imeandikwa, ‘Utamwabudu Bwana Mungu wako, nawe utamtumikia yeye peke yake.’ ”

11Ndipo ibilisi akamwacha, nao malaika wakaja na kumtumikia.

Yesu Aanza Kuhubiri

12Yesu aliposikia kwamba Yohana Mbatizaji alikuwa ametiwa gerezani, alirudi Galilaya. 13Akaondoka Nazareti akaenda kuishi Kapernaumu mji ulioko karibu na bahari, katika mipaka ya nchi ya Zabuloni na ya Naftali, 14ili kutimiza unabii wa nabii Isaya, kama alivyosema: 15“Nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali,
kwenye njia ya kuelekea baharini,
ng'ambo ya Yordani,
Galilaya ya watu Mataifa:
16watu wale waliokaa gizani
wameona nuru kuu
nao wale waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti,
nuru imewazukia.”17Tangu wakati huo, Yesu alianza kuhubiri akisema: “Tubuni, kwa maana Ufalme wa Mbinguni umekaribia.”

Yesu Awaita Wanafunzi Wake Wa Kwanza

18Wakati Yesu alipokuwa anatembea kando ya Bahari ya Galilaya aliwaona ndugu wawili, Simoni aitwaye Petro na Andrea ndugu yake. Walikuwa wakizitupa nyavu zao baharini kwa maana wao walikuwa wavuvi. 19Yesu akawaambia, “Njoni, nifuateni, nami nitawafanya muwe wavuvi wa watu.” 20Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata.

21Alipoendelea mbele kutoka pale, akawaona ndugu wengine wawili, Yakobo mwana wa Zebedayo na Yohana nduguye, wakiwa wamekaa kwenye mashua pamoja na baba yao Zebedayo wakiziandaa nyavu zao. Yesu akawaita. 22Nao mara wakaziacha nyavu zao, pamoja na baba yao, wakamfuata.

Yesu Ahubiri Na Kuponya Wagonjwa

23Yesu akapita katika Galilaya yote, akifundisha katika masinagogi yao, akihubiri habari njema za Ufalme wa Mungu, akiponya kila ugonjwa na kila aina ya maradhi miongoni mwa watu. 24Kwa hiyo sifa zake zikaenea sehemu zote za Shamu, nao watu wakamletea wote waliokuwa na magonjwa mbalimbali na maumivu, waliopagawa na pepo wachafu, wenye kifafa na waliopooza, naye akawaponya. 25Makutano makubwa ya watu yakawa yanamjia kutoka Galilaya, Dekapoli
4:25 Yaani Miji Kumi
, Yerusalemu, Uyahudi na kutoka ng'ambo ya Mto Yordani.

Copyright information for Neno