Micah 5

Mtawala Aliyeahidiwa Kutoka Bethlehemu

1 aPanga majeshi yako, ee mji wa majeshi,
kwa kuwa kuzingirwa kumepangwa dhidi yetu.
Watampiga mtawala wa Israeli
shavuni kwa fimbo.

2 b“Lakini wewe, Bethlehemu Efrathi,
ingawa u mdogo miongoni mwa koo za Yuda,
kutoka kwako atatokea kwa ajili yangu
yeye atakayekuwa mtawala katika Israeli,
ambaye asili yake ni kutoka zamani,
kutoka milele.”

3 cKwa hiyo Israeli utaachwa mpaka wakati
mwanamke aliye na utungu atakapozaa
na ndugu zake wengine warudi
kujiunga na Waisraeli.

4 dAtasimama na kulichunga kundi lake
katika nguvu ya Bwana,
katika utukufu wa jina la Bwana Mungu wake.
Nao wataishi kwa usalama, kwa kuwa wakati huo
ukuu wake utaenea hadi miisho ya dunia.
5 eNaye atakuwa amani yao.

Ukombozi Na Uharibifu

Wakati Mwashuru atakapovamia nchi yetu
na kupita katika ngome zetu,
tutawainua wachungaji saba dhidi yake,
hata viongozi wanane wa watu.
6 fWataitawala nchi ya Ashuru kwa upanga,
nchi ya Nimrodi kwa upanga.
Atatuokoa kutoka kwa Mwashuru
atakapoivamia nchi yetu
na kuingia katika mipaka yetu.

7 gMabaki ya Yakobo yatakuwa
katikati ya mataifa mengi
kama umande kutoka kwa Bwana,
kama manyunyu juu ya majani,
ambayo hayamngoji mtu
wala kukawia kwa mwanadamu.
8 hMabaki ya Yakobo yatakuwa miongoni mwa mataifa,
katikati ya mataifa mengi,
kama simba miongoni mwa wanyama wa msituni,
kama mwana simba miongoni
mwa makundi ya kondoo,
ambaye anaumiza vibaya na kuwararua
kila anapopita katikati yao,
wala hakuna awezaye kuokoa.
9 iMkono wako utainuliwa juu kwa ushindi juu ya watesi wako,
nao adui zako wote wataangamizwa.
10 j“Katika siku ile,” asema Bwana,

“nitaangamiza farasi zenu katikati yenu
na kubomoa magari yenu ya vita.
11 kNitaiangamiza miji ya nchi yenu
na kuziangusha chini ngome zenu zote.
12 lNitaangamiza uchawi wenu
na hamtapiga tena ramli.
13 mNitaangamiza vinyago vyenu vya kuchonga
na mawe yenu ya ibada yatoke katikati yenu;
hamtasujudia tena
kazi ya mikono yenu.
14 nNitangʼoa nguzo za Ashera katikati yenu
na kubomoa miji yenu.
15 oNitalipiza kisasi kwa hasira na ghadhabu
juu ya mataifa ambayo hayajanitii.”
Copyright information for SwhNEN