Micah 7

Taabu Ya Israeli

Taabu gani hii niliyo nayo!
Nimefanana na yule akusanyaye
matunda ya kiangazi,
aokotaye masazo baada ya kuvunwa
shamba la mizabibu;
hakuna kishada chenye matunda ya kula,
hakuna hata ile tini ya mwanzoni ninayoitamani.
Wanaomcha Mungu wameondolewa kutoka katika nchi;
hakuna mtu mnyofu hata mmoja aliyebaki.
Watu wote wanavizia kumwaga damu,
kila mmoja anamwinda ndugu yake kwa wavu.
Mikono yote miwili ni hodari katika kufanya ubaya,
mtawala anadai zawadi,
hakimu anapokea rushwa,
wenye nguvu wanaamuru wanachotaka:
wote wanafanya shauri baya pamoja.
Aliye mwema kupita wote kati yao
ni kama mchongoma,
anayeonekana mnyofu zaidi miongoni mwao
ni mbaya kuliko uzio wa miiba.
Siku ya walinzi wako imewadia,
siku atakayokutembelea Mungu.
Sasa ni wakati wao
wa kuchanganyikiwa.
Usimtumaini jirani;
usiweke matumaini kwa rafiki.
Hata kwa yule alalaye kifuani mwako
uwe mwangalifu kwa maneno yako.
Kwa kuwa mwana humdharau baba yake,
naye binti huinuka dhidi ya mama yake,
mkwe kuwa kinyume na mama mkwe wake:
adui wa mtu ni wale wa nyumbani mwake hasa.
Lakini mimi, namtazama BWANA kwa matumaini,
namngoja Mungu Mwokozi wangu;
Mungu wangu atanisikia mimi.

Israeli Atainuka

Usifurahie msiba wangu, Ee adui yangu!
Ingawa nimeanguka, nitainuka.
Japo ninaketi gizani,
BWANA atakuwa nuru yangu.
Kwa sababu nimetenda dhambi dhidi yake,
nitabeba ghadhabu ya BWANA,
mpaka atakaponitetea shauri langu
na kuithibitisha haki yangu.
Atanileta nje kwenye mwanga,
nami nitaiona haki yake.
10 Kisha adui yangu ataliona
naye atafunikwa na aibu,
yule aliyeniambia,
“Yu wapi BWANA Mungu wako?”
Macho yangu yataona kuanguka kwake,
hata sasa atakanyagwa chini ya mguu
kama tope barabarani.
11 Siku ya kujenga kuta zako itawadia,
siku ya kupanua mipaka yako.
12 Siku hiyo watu watakuja kwako
kutoka Ashuru na miji ya Misri,
hata kutoka Misri hadi Eufrati
na kutoka bahari hadi bahari
na kutoka mlima hadi mlima.
13 Dunia itakuwa ukiwa kwa sababu ya wakazi wake,
kwa sababu ya matunda ya matendo yao.

Sala Na Sifa

14 Wachunge watu wako kwa fimbo yako,
kundi la urithi wako,
ambalo linaishi peke yake msituni,
katika nchi ya malisho yenye rutuba.
Waache walishe katika Bashani na Gileadi
kama ilivyokuwa siku za kale.
15 “Kama siku zile mlipotoka Misri,
nitawaonyesha maajabu yangu.”
16 Mataifa yataona na kuaibika,
waliondolewa nguvu zao zote.
Wataweka mikono yao kwenye vinywa vyao
na masikio yao yatakuwa na uziwi.
17 Wataramba mavumbi kama nyoka,
kama viumbe vitambaavyo juu ya ardhi.
Watatoka nje ya mapango yao wakitetemeka;
watamgeukia BWANA Mungu wetu kwa hofu
nao watakuogopa.
18 Ni nani Mungu kama wewe,
ambaye anaachilia dhambi
na kusamehe makosa
ya mabaki ya urithi wake?
Wewe huwi na hasira milele,
bali unafurahia kuonyesha rehema.
19 Utatuhurumia tena,
utazikanyaga dhambi zetu
chini ya nyayo zako,
na kutupa maovu yetu yote
katika vilindi vya bahari.
20 Utakuwa wa kweli kwa Yakobo,
nawe utamwonyesha Abrahamu rehema,
kama ulivyowaahidi kwa kiapo baba zetu
siku za kale.
Copyright information for Neno