Nehemiah 12

Makuhani Na Walawi Waliorudi Na Zerubabeli

Hawa wafuatao walikuwa makuhani na Walawi ambao walirudi na Zerubabeli mwana wa Shealtieli pamoja na Yeshua:
  • Seraya, Yeremia, Ezra,
Amaria, Maluki, Hatushi, Shekania, Rehumu, Meremothi, Ido, Ginethoni, Abiya, Miyamini, Moadia, Bilga, Shemaya, Yoyaribu, Yedaya, Salu, Amoki, Hilkia na Yedaya. Hawa walikuwa viongozi wa makuhani na wenzao wakati wa Yeshua. Walawi walikuwa Yeshua, Binui, Kadmieli, Sherebia, Yuda, pia Matania, ambaye pamoja na wenzake, alikuwa kiongozi wa nyimbo za shukrani. Bakbukia na Uni, wenzao, walisimama mkabala nao wakati wa ibada.

10 Yeshua alikuwa baba wa Yoiakimu, Yoiakimu alikuwa baba wa Eliyashibu, Eliyashibu alikuwa baba wa Yoyada, 11 Yoyada alikuwa baba wa Yonathani, na Yonathani alikuwa baba wa Yadua.

12 Katika siku za Yoyakimu, kulikuwa na wakuu wa jamaa za kikuhani:
  • wa jamaa ya Seraya, Meraya;
  • wa Yeremia, Hamania;
13 wa jamaa ya Ezra, Meshulamu; wa jamaa ya Amaria, Yehohanani; 14 wa jamaa ya Maluki, Yonathani; wa jamaa ya Shekania, Yusufu; 15 wa jamaa ya Harimu, Helkai; 16 wa jamaa ya Ido, Zekaria; wa jamaa ya Ginethoni, Meshulamu; 17 wa jamaa ya Abia, Zikri; wa jamaa ya Miyamini na ya Maazia, Piltai; 18 wa jamaa ya Bilgai, Shamua; wa jamaa ya Shemaya, Yehonathani; 19 wa jamaa ya Yoyaribu, Matenai; wa jamaa ya Yedaya, Uzi; 20 wa jamaa ya Salu, Kalai; wajamaa ya Amoki, Eberi; 21 wa jamaa ya Hilkia, Hashabia; wa jamaa ya Yedaya, Nethaneli. 22 Wakuu wa jamaa za Walawi katika siku za Eliyashibu, Yoyada, Yohanani na Yadua, pia wale jamaa za makuhani, waliandikishwa wakati wa utawala wa Dario, Mwajemi. 23 Wakuu wa jamaa miongoni mwa wazao wa Lawi hadi wakati wa Yohanani mwana wa Eliyashibu waliandikishwa katika kitabu cha kumbukumbu. 24 Viongozi wa Walawi walikuwa: Hashabia, Sherebia, Yeshua mwana wa Kadmieli na wenzao, waliosimama mkabala nao kusifu na kushukuru, sehemu moja ikipokezana na nyingine kama ilivyoagizwa na Daudi mtu wa Mungu.

25 Mabawabu waliokuwa wakilinda kwenye malango ya ghala ni: Matania, Bakbukia, Obadia, Meshulamu, Talmoni na Akubu. 26 Walihudumu siku za Yoakimu mwana wa Yeshua, mwana wa Yozadaki, na katika siku za mtawala Nehemia na za Ezra kuhani na mwandishi.

Kuwekwa Wakfu Ukuta Wa Yerusalemu

27 Wakati wa kuwekwa wakfu ukuta wa Yerusalemu, Walawi walitafutwa huko walikokuwa wakiishi, nao wakaletwa Yerusalemu kuadhimisha kwa shangwe huko kuweka wakfu kwa nyimbo za shukrani na kwa uimbaji kwa kutumia matoazi, vinubi na zeze. 28 Pia waimbaji walikusanywa pamoja kutoka maeneo yanayozunguka Yerusalemu, kutoka vijiji vya Wanetofathi, 29 kutoka Beth-Gilgali, kutoka eneo la Geba na Azmawethi, kwa kuwa waimbaji walikuwa wamejijengea vijiji kuzunguka Yerusalemu. 30 Wakati makuhani na Walawi walipokuwa wamekwisha kujitakasa kwa kufuatana na desturi, waliwatakasa watu, malango na ukuta.

31 Niliwaagiza viongozi wa Yuda wapande juu ya ukuta. Pia niliagiza makundi mawili makubwa ya waimbaji waimbe nyimbo za kumshukuru Mungu. Moja lipande juu ya ukuta upande wa kuume, kuelekea Lango la Samadi. 32 Hoshaya na nusu ya viongozi wa Yuda wakawafuata, 33 pamoja na Azaria, Ezra, Meshulamu, 34 Yuda, Benyamini, Shemaya, Yeremia, 35 pamoja na baadhi ya makuhani wenye tarumbeta, pia walikuwa na Zekaria mwana wa Yonathani, mwana wa Shemaya, mwana wa Matania, mwana wa Mikaya, mwana wa Zakuri, mwana wa Asafu, 36 pamoja na wenzao, Shemaya, Azareli, Milalai, Gilalai, Maai, Nethaneli, Yuda na Hanani wakiwa na vyombo vya uimbaji, kama ilivyoagizwa na Daudi mtu wa Mungu. Mwandishi Ezra aliongoza maandamano. 37 Kwenye Lango la Chemchemi waliendelea moja kwa moja mpaka kwenye ngazi za Mji wa Daudi kwenye mwinuko wa ukuta na kupitia juu ya nyumba ya Daudi mpaka kwenye Lango la Maji upande wa mashariki.

38 Kundi la pili la waimbaji lilielekea upande wa kushoto. Niliwafuata juu ya ukuta, pamoja na nusu ya watu nyuma ya mnara wa Tanuru mpaka kwenye Ukuta Mpana, 39 juu ya Lango la Efraimu, Lango la Yeshana, Lango la Samaki, Mnara wa Hananeli na Mnara wa Mia, mpaka kwenye lango la Kondoo. Walipofika kwenye Lango la Ulinzi wakasimama.

40 Kisha yale makundi mawili ya waimbaji yaliyoshukuru yalichukua nafasi zao katika nyumba ya Mungu, nami pia, pamoja na nusu ya maafisa, 41 pamoja na makuhani wafuatao: Eliyakimu, Maaseya, Miniamini, Mikaya, Elioenai, Zekaria na Hanania wakiwa na tarumbeta zao, 42 pia Maaseya, Shemaya, Eleazari, Uzi, Yehohanani, Malkiya, Elamu na Ezeri. Makundi haya yaliimba chini ya uongozi wa Yezrahia. 43 Siku hiyo watu walitoa dhabihu nyingi, walishangilia kwa sababu Mungu aliwapa furaha kuu. Wanawake na watoto walishangilia pia. Sauti ya kushangilia huko Yerusalemu iliweza kusikika mbali sana.

44 Wakati huo watu walichaguliwa kuwa wasimamizi wa vyumba vya ghala kwa ajili ya matoleo, malimbuko na zaka. Kutoka kwenye yale mashamba yaliyozunguka miji walipaswa walete kwenye ghala mafungu kama sheria ilivyoamuru kwa ajili ya makuhani na Walawi, kwa kuwa Yuda alifurahishwa na huduma ya makuhani na Walawi. 45 Walifanya ibada ya Mungu wao na ibada ya utakaso, waimbaji na walinzi wa lango walifanya hivyo pia, kufuatana na amri za Daudi na Solomoni mwanawe. 46 Kwa muda mrefu uliopita, katika siku za Daudi na Asafu, walikuwepo viongozi wa waimbaji na wa nyimbo za sifa na za kumshukuru Mungu. 47 Kwa hiyo katika siku za Zerubabeli na za Nehemia, Israeli wote walitoa mafungu kila siku kwa ajili ya waimbaji na mabawabu. Pia walitenga fungu kwa ajili ya Walawi wengine, nao Walawi walitenga fungu kwa ajili ya wazao wa Aroni.

Copyright information for Neno