Nehemiah 2

Artashasta Amtuma Nehemia Yerusalemu

1Katika mwezi wa Nisani
2.1 Nisani (Abibu) ni mwezi wa kwanza katika kalenda ya Kiyunani; katika kalenda yetu ni Machi/Aprili
mwaka wa ishirini wa kutawala kwake Mfalme Artashasta, wakati divai ilipoletwa kwa ajili yake, niliichukua na kumpa mfalme. Sikuwahi kuonekana mwenye huzuni mbele yake kabla ya hapo.
2Basi mfalme akaniuliza, “Kwa nini uso wako unaonekana una huzuni wakati wewe si mgonjwa? Jambo hili si kitu kingine bali ni huzuni ya moyo.”

Niliogopa sana,
3lakini nikamwambia mfalme, “Mfalme na aishi milele! Kwa nini uso wangu usiwe na huzuni wakati mji walipozikwa baba zangu umebaki magofu na malango yake yameteketezwa kwa moto?”

4Mfalme akaniambia, “Je, haja yako ni nini?”

Ndipo nikaomba kwa Mungu wa mbinguni,
5nikamjibu mfalme, “Kama ikimpendeza mfalme na kama mtumishi wako amepata kibali machoni pake na anitume Yuda kwenye mji mahali baba zangu walipozikwa ili niweze kuujenga upya.”

6Kisha mfalme, pamoja na malkia akiwa ameketi karibu naye, akaniuliza, “Safari yako itachukua muda gani, nawe utarudi lini?” Ilimpendeza mfalme kunituma kwa hiyo nikapanga muda.

7Pia nikamwambia, “Kama ikimpendeza mfalme, naomba nipewe barua kwa watawala wa Ng'ambo ya Eufrati, ili wanipe ulinzi mpaka nifike Yuda. 8Naomba nipewe barua nipeleke kwa Asafu, mtunzaji wa msitu wa mfalme, ili anipe miti ya kutengeneza boriti kwa ajili ya malango ya ngome ya Hekalu, kwa ajili ya ukuta wa mji na makao yangu nitakapoishi.” Kwa kuwa mkono wenye neema wa Mungu wangu ulikuwa juu yangu, mfalme akanijalia ombi langu. 9Basi nilikwenda kwa watawala wa Ng'ambo ya Eufrati na kuwapa barua za mfalme. Pia mfalme alikuwa ametuma maafisa wa jeshi na askari wapanda farasi pamoja nami.

10Sanbalati Mhoroni na Tobia afisa Mwamoni waliposikia juu ya jambo hili, waliudhika sana kwamba amekuja mtu kuinua ustawi wa Waisraeli.

Nehemia Akagua Kuta Za Yerusalemu

11Nilikwenda Yerusalemu, nami baada ya kukaa huko siku tatu 12nikaondoka wakati wa usiku pamoja na watu wachache. Sikuwa nimemwambia mtu ye yote kile ambacho Mungu wangu alikuwa ameweka moyoni mwangu kufanya kwa ajili ya Yerusalemu. Hapakuwepo na mnyama ye yote pamoja nami isipokuwa yule niliyekuwa nimempanda.

13Nikatoka nje usiku kupitia Lango la Bondeni, kuelekea Kisima cha Joka na Lango la Samadi, nikikagua kuta za Yerusalemu, zilizokuwa zimebomolewa na malango yake yaliyokuwa yameteketezwa kwa moto. 14Kisha nikaelekea mpaka Lango la Chemchemi na Bwawa la Mfalme, lakini hapakuwepo nafasi ya kutosha kwa ajili ya mnyama wangu kupita, 15kwa hiyo nikapandia bondeni usiku, nikikagua ukuta. Mwishoni, nikarudi na kuingia tena kupitia Lango la Bondeni. 16Maafisa hawakujua nilikokwenda wala nilichokuwa nikifanya, kwa sababu mpaka sasa nilikuwa bado sijasema lo lote kwa Wayahudi wala makuhani wala wakuu wala maafisa wala mtu ye yote ambaye angefanya kazi.

17Ndipo nilipowaambia, “Mnaona taabu tuliyonayo: Yerusalemu imebaki magofu na malango yake yameteketezwa kwa moto. Njoni tujenge upya ukuta wa Yerusalemu, nasi hatutakuwa tena kwenye aibu hii.” 18Pia niliwaambia kuhusu mkono wenye neema wa Mungu wangu uliokuwa juu yangu na kile mfalme alichokuwa ameniambia.

Wakajibu, “Haya na tuanze kujenga tena.” Kwa hiyo wakaanza kazi hii njema.

19Lakini Sanbalati Mhoroni, Tobia afisa Mwamoni na Geshemu Mwarabu waliposikia kuhusu jambo hili, walitudhihaki na kutucheka. Wakauliza, “Ni nini hiki mnachokifanya? Je, mnaasi dhidi ya mfalme?”

20Nikawajibu kwa kusema, “Mungu wa mbinguni atatufanikisha. Sisi watumishi wake tutaanza kujenga upya, lakini kwenu ninyi, hamna sehemu wala dai lo lote wala kumbukumbu la haki katika Yerusalemu.”

Copyright information for Neno