Nehemiah 6

Upinzani Zaidi Wakati Wa Ujenzi

1Habari zilipofika kwa Sanbalati, Tobia, Geshemu Mwarabu na adui zetu wengine kwamba nimejenga tena ukuta na hakuna nafasi iliyobakia ndani mwake, ingawa mpaka wakati huo sikuwa nimeweka milango kwenye malango, 2Sanbalati na Geshemu wakanipelekea ujumbe huu: “Njoo, tukutane katika mojawapo ya vijiji katika nchi tambarare ya Ono.”

Lakini walikuwa wakikusudia kunidhuru,
3kwa hiyo niliwatuma wajumbe kwao na majibu haya: “Kazi ninayoifanya ni kubwa sana siwezi kuja. Kwa nini niiache kazi isimame nije kwenu?” 4Mara nne walinitumia ujumbe wa namna iyo hiyo na kila mara niliwapa jibu lile lile.

5Basi, mara ya tano, Sanbalati akamtuma msaidizi wake kwangu akiwa na ujumbe wa aina ile ile, naye alikuwa amechukuwa mkononi mwake barua isiyofungwa, 6iliyokuwa imeandikwa:“Habari imeenezwa miongoni mwa mataifa naye Geshemu anasema kwamba ni kweli, kuwa wewe na Wayahudi mnafanya hila ya kuasi, ndiyo sababu mnajenga ukuta. Zaidi ya hayo, kwa kufuatana na taarifa hizi karibu utakuwa mfalme wao
7na hata umewateua manabii wafanye tangazo hili kukuhusu wewe huko Yerusalemu: ‘Yuko mfalme katika Yuda!’ Sasa taarifa hii itarudishwa kwa mfalme; basi njoo, tufanye shauri pamoja.”8Nilimpelekea jibu hili: “Hakuna jambo kama hilo unalosema linalofanyika; unalitunga tu kwenye kichwa chako.”

9Wote walikuwa wakijaribu kutuogopesha, wakifikiri kuwa, “Mikono ya watu italegea kiasi kwamba hawataweza kufanya kazi, nayo haitakamilika.”

Lakini niliomba, “Ee Mungu, sasa nitie mikono yangu nguvu.”

10Siku moja nilikwenda nyumbani kwa Shemaya mwana wa Delaya, mwana wa Mehetabeli, ambaye alikuwa amefungwa ndani ya nyumba yake. Akasema, “Tukutane katika nyumba ya Mungu, ndani ya Hekalu na tufunge milango ya Hekalu, kwa sababu watu wanakuja kukuua. Naam, usiku wanakuja kukuua.”

11Lakini nikasema, “Je, mtu kama mimi akimbie? Au mtu kama mimi aende Hekaluni kuokoa maisha yake? Sitakwenda!” 12Nilitambua kwamba Mungu hakumtuma, bali alitabiri dhidi yangu kwa sababu Tobia na Sanbalati walikuwa wamemwajiri. 13Alikuwa ameajiriwa kunitisha ili kwa kufanya jambo hili nitende dhambi, kisha waweze kuniharibia jina langu na kuniaibisha.14Ee Mungu wangu, wakumbuke Tobia na Sanbalati kwa sababu ya yale waliyotenda, pia kumbuka nabii mke Noadia na manabii wengine ambao wamekuwa wakijaribu kunitisha.

Kukamilika Kwa Ukuta

15Basi ukuta ukakamilika siku ya ishirini na tano mwezi wa Eluli
6.15 Eluli ni mwezi wa sita kwenye kalenda ya Kiyunani; katika kalenda yetu ni Agosti/Septemba
, kazi ambayo ilichukua siku hamsini na mbili.
16Adui zetu wote waliposikia kuhusu hili, mataifa yote yaliyotuzunguka yakaogopa na kupoteza ujasiri, kwa sababu yalitambua kuwa kazi hii imefanyika kwa msaada wa Mungu wetu.

17Pia, katika siku hizo wakuu wa Yuda walikuwa wakituma barua nyingi kwa Tobia, nayo majibu yaliyotoka kwa Tobia yaliendelea kuwajia. 18Kwa kuwa watu wengi katika Yuda walikuwa wamemwapia Tobia, kwani alikuwa mkwewe Shekania mwana wa Ara, naye ni mwanawe Yehohanani aliyekuwa amemwoa binti wa Meshulamu mwana wa Berekia. 19Zaidi ya hayo walikuwa wakiniarifu jinsi Tobia alivyo mtu mwema, nao walimwambia kila kitu nilichosema. Naye Tobia alituma barua za kunitisha.

Copyright information for Neno