Numbers 23

Ujumbe Wa Kwanza Wa Balaamu

1 aBalaamu akasema, “Nijengee hapa madhabahu saba, mnitayarishie mafahali saba na kondoo dume saba.” 2Balaki akafanya kama Balaamu alivyosema; hao wawili kila mmoja wao akatoa fahali mmoja na kondoo dume mmoja juu ya kila madhabahu.

3 bKisha Balaamu akamwambia Balaki, “Kaa hapa kando ya sadaka yako wakati mimi ninakwenda kando. Huenda Bwana atakuja kukutana nami. Lolote atakalonifunulia, nitakuambia.” Basi akaenda hata mahali peupe palipoinuka.

4 cMungu akakutana naye, kisha Balaamu akasema, “Nimekwisha kutengeneza madhabahu saba, na juu ya kila madhabahu nimetoa sadaka ya fahali mmoja na kondoo dume mmoja.”

5 d Bwana akaweka ujumbe katika kinywa cha Balaamu na kusema, “Rudi kwa Balaki umpe ujumbe huu.”

6 eBasi Balaamu akarudi kwa Balaki, akamkuta amesimama kando ya sadaka yake akiwa na wakuu wote wa Moabu. 7 fNdipo Balaamu akasema ujumbe wake:

“Balaki amenileta kutoka Aramu,
mfalme wa Moabu kutoka milima ya mashariki.
Akasema, ‘Njoo, unilaanie Yakobo;
njoo unishutumie Israeli.’
8 gNitawezaje kuwalaani,
hao ambao Mungu hajawalaani?
Nitawezaje kuwashutumu
hao ambao Bwana hakuwashutumu?
9 hKutoka vilele vya miamba ninawaona,
kutoka mahali palipoinuka ninawatazama.
Ninaliona taifa ambalo wanaishi peke yao,
nao hawahesabiwi kama mojawapo ya mataifa.
10 iNi nani awezaye kuhesabu mavumbi ya Yakobo,
au kuhesabu robo ya Israeli?
Mimi na nife kifo cha mtu mwenye haki,
na mwisho wangu na uwe kama wao!”
11Balaki akamwambia Balaamu, “Ni nini ulichonitendea? Nimekuleta ulaani adui zangu, lakini wewe badala yake umewabariki!”

12Balaamu akajibu, “Je, hainipasi kusema kile Bwana anachoweka katika kinywa changu?”

Ujumbe Wa Pili Wa Balaamu

13Ndipo Balaki akamwambia, “Twende pamoja mahali pengine ambapo unaweza kuwaona; utawaona baadhi tu wala si wote. Nawe kutoka huko, unilaanie hao.” 14 jBasi akampeleka kwenye shamba la Sofimu, juu ya kilele cha Mlima Pisga. Pale akajenga madhabahu saba na kutoa sadaka ya fahali na kondoo dume mmoja juu ya kila madhabahu.

15Balaamu akamwambia Balaki, “Kaa hapa kando ya sadaka yako wakati ninapokwenda kuonana na Mungu kule.”

16 Bwana akakutana na Balaamu, akaweka ujumbe katika kinywa chake akasema, “Rudi kwa Balaki umpe ujumbe huu.”

17 kBasi Balaamu akarudi kwa Balaki, akamkuta amesimama kando ya sadaka yake, akiwa na wakuu wa Moabu. Balaki akamuuliza, “Je, Bwana amesema nini?”

18 lNdipo Balaamu akasema ujumbe wake:

“Balaki, inuka na usikilize,
nisikie mimi, wewe mwana wa Sipori.
19 mMungu si mtu, hata aseme uongo,
wala yeye si mwanadamu, hata ajute.
Je, anasema, kisha asitende?
Je, anaahidi, asitimize?
20Nimepokea agizo kubariki;
amebariki, nami siwezi kubadilisha.

21“Haijaonekana bahati mbaya katika Yakobo,
wala taabu katika Israeli.
Bwana, Mungu wao yu pamoja nao,
nayo sauti kuu ya Mfalme imo katikati yao.
22Mungu aliwatoa kutoka Misri;
wao wana nguvu za nyati.
23Hakuna uchawi dhidi ya Yakobo,
wala hakuna uaguzi dhidi ya Israeli.
Sasa itasemwa kuhusu Yakobo
na Israeli, ‘Tazama yale Mungu aliyotenda!’
24Taifa lainuka kama simba jike;
linajiinua kama simba
ambaye hatulii mpaka amalize kurarua mawindo yake
na kunywa damu ya mawindo yake.”
25Kisha Balaki akamwambia Balaamu, “Usiwalaani kabisa, wala usiwabariki kabisa!”

26Balaamu akajibu, “Je, sikukuambia ni lazima nifanye lolote analosema Bwana?”

Ujumbe Wa Tatu Wa Balaamu

27Basi Balaki akamwambia Balaamu, “Njoo, nikupeleke mahali pengine. Huenda itampendeza Mungu kukuruhusu unilaanie hao watu kutoka mahali hapo.” 28Balaki akamchukua Balaamu juu ya Mlima Peori, unaotazamana na nyika.

29Balaamu akasema, “Nijengee hapa madhabahu saba, uandae mafahali saba na kondoo dume saba kwa ajili yangu.” 30Balaki akafanya kama Balaamu alivyosema, kisha akatoa sadaka ya fahali mmoja na kondoo dume mmoja juu ya kila madhabahu.

Copyright information for SwhNEN