Numbers 30

Nadhiri

Mose akawaambia viongozi wa makabila ya Israeli: “Hili ndilo BWANA analoagiza: Wakati mwanaume awekapo nadhiri kwa BWANA, au anapoapa kujifunga kwa ahadi, kamwe asitangue neno lake, bali ni lazima afanye kila kitu alichosema.

“Wakati mwanamwali anayeishi bado nyumbani kwa baba yake atakapoweka nadhiri kwa BWANA, ama amejifunga mwenyewe kwa ahadi, na baba yake akasikia kuhusu nadhiri au ahadi yake lakini asimwambie lo lote, ndipo nadhiri zake zote na kila ahadi aliyoiweka na kujifunga kwayo itathibitika. Lakini kama baba yake akimkataza wakati anapoisikia, hakuna nadhiri wala ahadi yake ye yote aliyojifunga kwayo itakayosimama; BWANA atamwacha huru huyo mwanamwali kwa sababu baba yake amemkataza.

“Ikiwa ataolewa baada ya kuweka nadhiri au baada ya midomo yake kutamka ahadi fulani bila kufikiri akawa amejifunga hivyo, na mume wake akasikia habari hiyo asimwambie neno lo lote, ndipo nadhiri zake ama ahadi zake ambazo alikuwa amejifunga nazo zitathibitika. Lakini ikiwa mume wake atamkataza atakaposikia kuhusu hilo, atakuwa ametangua nadhiri ambazo zilikuwa zimemfunga mkewe, ama ahadi aliyotamka pasipo kufikiri ambayo amejifunga kwayo, naye BWANA atamwacha huru yule mwanamke.

“Nadhiri yo yote ama patano ambalo limefanywa na mjane ama mwanamke aliyeachika vitakuwa vimemfunga.

10 “Ikiwa mwanamke anayeishi na mumewe ataweka nadhiri ama kujifunga mwenyewe kwa ahadi chini ya kiapo, 11 na mumewe akasikia kuhusu jambo hili lakini asimwambie lo lote wala hakumkataza, ndipo viapo vyake vyote au ahadi zinazomfunga zitakapothibitika. 12 Lakini ikiwa mumewe atabatilisha nadhiri hizo baada ya kuzisikia, basi hakuna nadhiri au ahadi zo zote alizoziweka kwa midomo yake zitakazothibitika. Mumewe atakuwa amezibatilisha, na BWANA atamweka huru yule mwanamke. 13 Mumewe anaweza kuthibitisha au kutangua nadhiri ye yote anayoweka, au ahadi ye yote aliyoweka kwa kuapa ili kujikana mwenyewe. 14 Lakini ikiwa mumewe hasemi lo lote kwake kuhusu jambo hilo siku baada ya siku, basi mumewe atakuwa amethibitisha nadhiri zote, na ahadi zote zinazomfunga mkewe. Anavithibitisha kwa kutokusema lo lote kwa mkewe anapoyasikia hayo. 15 Hata hivyo, ikiwa mumewe atavibatilisha baada ya kusikia hayo, basi atawajibika kwa hatia ya mkewe.”

16 Haya ndiyo masharti ambayo BWANA alimpa Mose kuhusu mahusiano kati ya mtu na mkewe, na kati ya baba na binti yake ambaye bado anaishi nyumbani kwa baba yake.

Copyright information for Neno