FILEMONI

Filemoni

Utangulizi

Waraka huu mfupi umeainishwa na nyaraka za Waefeso, Wakolosai na Wafilipi kama mojawapo ya nyaraka zake za gerezani. Ameandikiwa Filemoni, Afia mwanamke Mkristo (ambaye huenda alikuwa mkewe Filemoni), na Arkipo na kanisa lililokuwa likikusanyika nyumbani kwa Filemoni.

Onesmo alikuwa mtumwa aliyetoroka kutoka kwa Filemoni huko Kolosai kwenda Rumi, ambako aliongoka. Onesimo kama mtumwa alikuwa mali ya Filemoni kisheria.Wazo Kuu

Paulo anamwandikia Filemoni kumshawishi amkubali Onesimo tena na amsamehe kama alikuwa amemkosea.Mwandishi

Mtume Paulo.Kusudi

Kumhimiza Filemoni amsamehe Onesmo, mtumwa aliyemtoroka, na amkubali kama ndugu Mkristo katika imani.Mambo Muhimu

Barua hii ni kielelezo cha ukarimu wa Kikristo. Paulo anaanza kwa shukrani kwa moyo wa ukarimu ambao tayari Filemoni alikuwa ameonyesha kwa Wakristo wenzake. Paulo kwa mamlaka yake aliokuwa nayo katika kanisa angeweza kumtaka afanye hivyo kwa Onesmo. Badala yake Paulo anaomba kwa upendo Filemoni ampokee Onesmo.Mahali

Rumi.Tarehe

Kama mwaka wa 60 B.K.Wahusika Wakuu

Paulo, Filemoni na Onesmo.Mgawanyo

  • • Salamu (1:1-3)
  • • Kuhusika kwa Paulo na upendo wake (1:4-7)
  • • Paulo kumwombea Onesmo (1:8-22)
  • • Kuagana (1:23-25).

Philemon

1Paulo, mfungwa wa Kristo Yesu, pamoja na Timotheo ndugu yetu:

Kwa Filemoni rafiki yetu mpendwa na mtenda kazi mwenzetu,
2kwa dada yetu mpendwa Afia, kwa Arkipo askari mwenzetu na kwa kanisa lile likutanalo nyumbani mwako:

3Neema iwe nanyi na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo.

Shukrani Na Maombi

4Siku zote ninamshukuru Mungu ninapokukumbuka katika maombi yangu, 5kwa sababu ninasikia juu ya imani yako katika Bwana Yesu na upendo wako kwa watakatifu wote. 6Naomba utiwe nguvu katika kuishuhudia imani yako, ili upate kuwa na ufahamu mkamilifu juu ya kila kitu chema tulicho nacho ndani ya Kristo. 7Upendo wako umenifurahisha mno na kunitia moyo, kwa sababu wewe ndugu, umeiburudisha mioyo ya watakatifu.

Maombi Ya Paulo Ya Kumtetea Onesmo

8Hata hivyo, ingawa katika Kristo ningeweza kuwa na ujasiri na kukuagiza yale yakupasayo kutenda, 9lakini ninakuomba kwa upendo, mimi Paulo, mzee na pia sasa nikiwa mfungwa wa Kristo Yesu, 10nakuomba kwa ajili ya mwanangu Onesmo
1:10 Onesmo maana yake ni Wa manufaa
, aliyefanyika mwanangu nilipokuwa kwenye minyororo.
11Mwanzoni alikuwa hakufai, lakini sasa anakufaa sana wewe na mimi pia.

12Namtuma kwako, yeye aliye moyo wangu hasa. 13Ningependa nikae naye ili ashike nafasi yako ya kunisaidia wakati huu nikiwa kifungoni kwa ajili ya Injili. 14Lakini sikutaka kufanya lo lote bila idhini yako, ili wema wo wote uufanyao usiwe wa lazima, bali wa hiari. 15Huenda sababu ya yeye kutengwa nawe kwa kitambo kidogo ni ili uwe naye daima. 16Si kama mtumwa, bali bora kuliko mtumwa, kama ndugu mpendwa. Yeye ni mpendwa sana kwangu na hata kwako zaidi, yeye kama mwanadamu na kama ndugu katika Bwana.

17Hivyo kama unanihesabu mimi kuwa mshirika wako, mkaribishe kama vile ungenikaribisha mimi mwenyewe. 18Kama amekukosea lo lote au kama unamdai cho chote, nidai mimi. 19Mimi Paulo, ninaandika waraka huu kwa mkono wangu mwenyewe, mimi nitalipa. Si kwamba ninakudai hata nafsi yako mwenyewe. 20Ndugu yangu, natamani nipate faida kwako katika Bwana, uuburudishe moyo wangu katika Kristo. 21Nikiwa na hakika ya utii wako, nakuandikia, nikijua kwamba utafanya hata zaidi ya yale nisemayo.

22Jambo moja zaidi: Niandalie chumba cha wageni, kwa kuwa nataraji kurudishwa kwenu kama jibu la maombi yenu.

Salamu Za Mwisho Na Dua Ya Kuwatakia Heri

23Epafra, aliye mfungwa mwenzangu katika Kristo Yesu, anakusalimu. 24Vivyo hivyo Marko, Aristarko, Dema na Luka, watenda kazi wenzangu wanakusalimu.

25Neema ya Bwana Yesu Kristo iwe pamoja na roho zenu. Amen.

Copyright information for Neno