Proverbs 31

Mithali Za Mfalme Lemueli

Mithali za Mfalme Lamueli, mausia ya mama yake aliyomfundisha:

“Ee mwanangu, Ee mwana wa tumbo langu,
Ee mwana wa nadhiri zangu
31.2 Au: Ewe uliye jibu la maombi yangu
,
Usitumie nguvu zako kwa wanawake,
uhodari wako kwa wale wanaowaharibu wafalme.
“Ee Lemueli, haifai wafalme,
haifai wafalme kunywa mvinyo,
haifai watawala kutamani sana kileo,
wasije wakanywa na kusahau ile sheria inayoamuru
na kuwanyima haki zao wote walioonewa.
Wape kileo wale wanaoangamia,
mvinyo wale walio na uchungu,
Wanywe na kusahau umaskini wao
na wasikumbuke taabu yao tena.
“Sema kwa ajili ya wale wasioweza kujisemea,
kwa ajili ya haki za wote walioachwa ukiwa.
Sema na uamue kwa haki,
tetea haki za maskini na wahitaji.”


Maneno Ya Mwisho: Mke Mwenye Sifa Nzuri
31:9 Methaali 31:10-31 imetungwa kila mstari ukianzia na herufi ya alfabeti ya Kiebrania zikifuatana tangu Aleph (A) hadi Taw (T); zote ni 22

10 Mke mwenye sifa nzuri, ni nani awezaye kumpata?
Yeye ni wa thamani sana kuliko marijani.
11 Mume wake anamwamini kikamilifu
wala hakosi kitu cho chote cha thamani.
12 Humtendea mumewe mema, wala si mabaya,
siku zote za maisha yake.
13 Huchagua sufu na kitani
naye hufanya kazi kwa mikono yenye bidii.
14 Yeye ni kama meli za biashara
akileta chakula chake kutoka mbali.
15 Yeye huamka kungali bado giza
huwapa jamaa yake chakula
na mafungu kwa watumishi wake wa kike.
16 Huangalia shamba na kulinunua,
kutokana na mapato yake hupanda shamba la mizabibu.
17 Hufanya kazi zake kwa nguvu,
mikono yake ina nguvu kwa ajili ya kazi zake.
18 Huona kwamba biashara yake ina faida,
wala taa yake haizimiki usiku.
19 Huweka mikono yake kwenye pia,
navyo vidole vyake hushikilia kijiti chenye uzi.
20 Huwanyoshea maskini mikono yake
na kuwakunjulia wahitaji vitanga vyake.
21 Theluji ishukapo, hana hofu kwa ajili ya watu wa nyumbani mwake,
kwa maana wote wamevikwa nguo za kutia joto.
22 Hutengeneza mazulia ya urembo ya kufunika kitanda chake,
yeye huvaa kitani safi na urujuani.
23 Mume wake anaheshimiwa kwenye lango la mji,
aketipo miongoni mwa wazee wa nchi.
24 Hutengeneza mavazi ya kitani na kuyauza,
naye huwauzia wafanyabiashara mishipi.
25 Amevikwa nguvu na heshima,
anaweza kucheka bila kuwa na hofu kwa siku zijazo.
26 Huzungumza kwa hekima
na mafundisho ya kuaminika yapo ulimini mwake.
27 Huangalia mambo ya nyumbani mwake
wala hali chakula cha uvivu.
28 Watoto wake huamka na kumwita mbarikiwa
na mumewe pia, naye humsifu:
29 “Wanawake wengi hufanya vitu vyenye sifa nzuri,
lakini wewe umewapita wote.”
30 Kujipamba ili kuvutia ni udanganyifu, uzuri unapita upesi,
bali mwanamke anayemcha BWANA atasifiwa.
31 Mpe thawabu anayostahili,
nazo kazi zake na zimletee sifa kwenye lango la mji.
Copyright information for Neno