Psalms 103

Upendo Wa Mungu

(Zaburi Ya Daudi)

1Ee nafsi yangu, umhimidi BWANA,
vyote vilivyomo ndani yangu
vilihimidi jina lake takatifu.
2Ee nafsi yangu, umhimidi BWANA,
wala usisahau wema wake wote,
3akusamehe dhambi zako zote,
akuponya magonjwa yako yote,
4aukomboa uhai wako na kaburi,
akuvika taji ya upendo na huruma,
5atosheleza mahitaji yako kwa vitu vyema,
ili ujana wako uhuishwe kama wa tai.
6BWANA hutenda haki,
naye huwapa hukumu ya haki
wote wanaoonewa.
7Alimjulisha Mose njia zake,
matendo yake kwa wana wa Israeli.
8BWANA ni mwenye huruma na rehema,
si mwepesi wa hasira,
amejaa upendo.
9Yeye hatalaumu siku zote,
wala haweki hasira yake milele,
10yeye hatutendei kulingana na dhambi zetu
wala hatupatilizi kwa kadiri ya maovu yetu.
11Kama vile mbingu zilivyo juu sana juu ya dunia,
ndivyo wema wake ulivyo mwingi
kwa wanaomcha;
12kama mashariki ilivyo mbali na magharibi,
ndivyo Mungu alivyoziweka
dhambi zetu mbali nasi.
13Kama baba alivyo na huruma kwa watoto wake,
ndivyo BWANA anavyowahurumia
wale wanaomcha;
14kwa kuwa anajua tulivyoumbwa,
anakumbuka kwamba sisi tu mavumbi.
15Kuhusu mwanadamu, siku zake ni kama majani,
anachanua kama ua la shambani;
16upepo huvuma juu yake nalo hutoweka,
mahali pake hapalikumbuki tena.
17Lakini kutoka milele hata milele
upendo wa BWANA uko kwa wale wamchao,
nayo haki yake kwa watoto wa watoto wao:
18kwa wale walishikao Agano lake
na kukumbuka kuyatii mausia yake.
19BWANA ameweka imara kiti chake cha enzi mbinguni,
ufalme wake unatawala juu ya vyote.
20Mhimidini BWANA, enyi malaika zake,
ninyi mlio mashujaa mnaozitii amri zake,
ninyi mnaotii neno lake.
21Mhimidini BWANA, ninyi jeshi lake lote la mbinguni,
ninyi watumishi wake mnaofanya mapenzi yake.
22Mhimidini BWANA, kazi zake zote
kila mahali katika milki yake.
Ee nafsi yangu, umhimidi BWANA.
Copyright information for Neno