Psalms 105

Uaminifu Wa Mungu Kwa Israeli

(1 Nya 16:8-22)

Mshukuruni BWANA, liitieni jina lake,
wajulisheni mataifa yale aliyoyatenda.
Mwimbieni yeye, mwimbieni yeye sifa,
waambieni matendo yake yote ya ajabu.
Utukufu kwa jina lake takatifu,
mioyo ya wale wamtafutao BWANA na ifurahi.
Mtafuteni BWANA na nguvu zake,
utafuteni uso wake siku zote.
Kumbuka matendo ya ajabu aliyoyafanya,
miujiza yake na hukumu alizozitamka.
Enyi wazao wa Abrahamu mtumishi wake,
Enyi wana wa Yakobo, wateule wake.
Yeye ndiye BWANA Mungu wetu,
hukumu zake zimo duniani pote.
Hulikumbuka Agano lake milele,
neno ambalo aliamuru, kwa vizazi elfu,
Agano alilolifanya na Abrahamu,
kiapo alichomwapia Isaki.
10 Alilithibitisha kwa Yakobo kama amri,
kwa Israeli kama Agano la milele:
11 “Wewe nitakupa nchi ya Kanaani
kama sehemu utakayoirithi.”
12 Walipokuwa wachache kwa idadi,
wachache sana na wageni ndani yake,
13 walitangatanga kutoka taifa moja hadi jingine,
kutoka ufalme mmoja hadi mwingine.
14 Hakuruhusu mtu ye yote awaonee,
kwa ajili yao aliwakemea wafalme,
15 akisema, “Msiwaguse masiya wangu,
msiwadhuru manabii wangu.”
16 Akaiita njaa juu ya nchi
na kuharibu chakula chao chote,
17 naye akatuma mtu mbele yao,
Yosefu, aliyeuzwa kama mtumwa.
18 Walichubua miguu yake kwa minyororo,
shingo yake ilifungwa kwa chuma,
19 mpaka yale aliyotangulia kusema yalipotimia,
mpaka neno la BWANA lilipomjaribu
na kumthibitisha.
20 Mfalme alituma akamfungua,
mtawala wa watu alimwachia huru.
21 Alimfanya mkuu wa nyumba yake,
mtawala juu ya vyote alivyokuwa navyo,
22 kuwaelekeza wakuu wa mfalme apendavyo
na kuwafundisha wazee wake hekima.
23 Kisha Israeli akaingia Misri,
Yakobo akaishi kama mgeni
katika nchi ya Hamu.
24 BWANA aliwafanya watu wake kuzaana sana,
akawafanya kuwa wengi sana
kuliko adui zao,
25 ndiye aliyeigeuza mioyo yao iwachukie watu wake,
wakatenda hila dhidi ya watumishi wake.
26 Akamtuma Mose mtumishi wake,
pamoja na Aroni,
ambaye alikuwa amemchagua.
27 Walifanya ishara zake za ajabu miongoni mwao,
miujiza yake katika nchi ya Hamu.
28 Alituma giza na nchi ikawa giza,
kwani si walikuwa wameyaasi maneno yake?
29 Aligeuza maji yao kuwa damu,
ikasababisha samaki wao kufa.
30 Nchi yao ilijaa vyura tele,
ambao waliingia
hadi kwenye vyumba vya kulala
vya watawala wao.
31 Alisema, yakaja makundi ya mainzi,
na viroboto katika nchi yao yote.
32 Alibadilisha mvua yao ikawa mvua ya mawe,
yenye umeme wa radi katika nchi yao yote,
33 akaharibu mizabibu yao na miti ya tini
na akaangamiza miti ya nchi yao.
34 Alisema, nzige wakaja,
tunutu wasio na idadi,
35 wakala kila kitu cha kijani kibichi katika nchi yao,
wakala mazao ya ardhi yao.
36 Kisha akawaua wazaliwa wote wa kwanza
katika nchi yao,
matunda ya kwanza ya ujana wao wote.
37 Akawatoa Israeli katika nchi
wakiwa na fedha
na dhahabu nyingi,
wala hakuna hata mmoja
kutoka katika kabila zao aliyejikwaa.
38 Misri ilifurahi walipoondoka,
kwa sababu hofu ya Israeli
ilikuwa imewaangukia.
39 Alitandaza wingu kama kifuniko
na moto kuwamulikia usiku.
40 Waliomba, naye akawaletea kware,
akawashibisha kwa mkate wa mbinguni.
41 Alipasua mwamba, maji yakabubujika,
yakatiririka jangwani kama mto.
42 Kwa maana alikumbuka ahadi yake takatifu,
aliyompa Abrahamu mtumishi wake.
43 Aliwatoa watu wake kwa furaha,
wateule wake kwa kelele za shangwe,
44 akawapa nchi za mataifa,
wakawa warithi wa vitu
ambavyo wengine
walikuwa wamevitaabikia,
45 alifanya haya ili wayashike mausia yake
na kuzitii sheria zake.
Msifuni BWANA
105.45 Msifuni BWANA kwa Kiebrania ni Hallelu Yah
.
Copyright information for Neno