Psalms 136

Wimbo Wa Kumshukuru Mungu

Mshukuruni BWANA, kwa kuwa ni mwema.
Fadhili zake zadumu milele.

Mshukuruni Mungu wa miungu.
Fadhili zake zadumu milele.

Mshukuruni Bwana wa mabwana:
Fadhili zake zadumu milele.

Kwake yeye pekee atendaye maajabu makuu,
Fadhili zake zadumu milele.

Ambaye kwa ufahamu wake aliziumba mbingu,
Fadhili zake zadumu milele.

Ambaye aliitandaza dunia juu ya maji,
Fadhili zake zadumu milele.

Ambaye aliumba mianga mikubwa,
Fadhili zake zadumu milele.

Jua litawale mchana,
Fadhili zake zadumu milele.

Mwezi na nyota vitawale usiku,
Fadhili zake zadumu milele.

10 Kwake yeye aliyemwua mzaliwa wa kwanza wa Misri,
Fadhili zake zadumu milele.

11 Na kuwatoa Israeli katikati yao,
Fadhili zake zadumu milele.

12 Kwa mkono wenye nguvu ulionyooshwa,
Fadhili zake zadumu milele.

13 Kwake yeye aliyeigawa Bahari ya Shamu,
Fadhili zake zadumu milele.

14 Na kuwapitisha Israeli katikati yake,
Fadhili zake zadumu milele.

15 Lakini alimfagia Farao na jeshi lake katika Bahari ya Shamu,
Fadhili zake zadumu milele.

16 Kwake yeye aliyewaongoza watu wake katika jangwa,
Fadhili zake zadumu milele.

17 Ambaye aliwapiga wafalme wenye nguvu,
Fadhili zake zadumu milele.

18 Naye aliwaua wafalme wenye nguvu,
Fadhili zake zadumu milele.

19 Sihoni mfalme wa Waamori,
Fadhili zake zadumu milele.

20 Ogu mfalme wa Bashani,
Fadhili zake zadumu milele.

21 Akatoa nchi yao kuwa urithi,
Fadhili zake zadumu milele.

22 Urithi kwa Israeli mtumishi wake,
Fadhili zake zadumu milele.

23 Aliyetukumbuka katika unyonge wetu,
Fadhili zake zadumu milele.

24 Alituweka huru toka adui zetu,
Fadhili zake zadumu milele.

25 Ambaye humpa chakula kila kiumbe.
Fadhili zake zadumu milele.

26 Mshukuruni Mungu wa mbinguni,
Fadhili zake zadumu milele.

Copyright information for Neno