Psalms 139

Mungu Asiyeweza Kukwepwa

(Kwa Mwimbishaji: Zaburi Ya Daudi)

1Ee BWANA, umenichunguza
na kunijua.
2Unajua ninapoketi na ninapoinuka;
unatambua mawazo yangu tokea mbali.
3Unafahamu kutoka kwangu na kulala kwangu;
unaelewa njia zangu zote.
4Kabla neno halijafika katika ulimi wangu,
wewe walijua kikamilifu, Ee BWANA.
5Umenizunguka nyuma na mbele;
umeweka mkono wako juu yangu.
6Maarifa haya ni ya ajabu mno kwangu,
ni ya juu sana kwangu kuyafikia.
7Niende wapi nijiepushe na Roho yako?
Niende wapi niukimbie uso wako?
8Kama nikienda juu mbinguni, wewe uko huko;
nikifanya vilindi
139.8 Vilindi ina maana ya Kuzimu, ambayo ni Sheol kwa Kiebrania
kuwa kitanda changu,
wewe uko huko.
9Kama nikipanda juu ya mbawa za mapambazuko,
kama nikikaa pande za mbali za bahari,
10hata huko mkono wako utaniongoza,
mkono wako wa kuume
utanishika kwa uthabiti.
11Kama nikisema, “Hakika giza litanificha
na nuru inayonizunguka iwe usiku,”
12hata giza halitakuwa giza kwako,
usiku utang'aa kama mchana,
kwa kuwa giza ni kama nuru kwako.
13Kwa maana wewe ndiwe uliyeumba
utu wangu wa ndani;
uliniunga pamoja tumboni
mwa mama yangu.
14Ninakusifu kwa sababu nimeumbwa
kwa namna ya ajabu na ya kutisha;
kazi zako ni za ajabu,
ninajua hayo kikamilifu.
15Umbile langu halikufichika kwako,
nilipoumbwa mahali pa siri.
Nilipoungwa pamoja kwa ustadi
katika vilindi vya nchi,
16macho yako yaliniona
kabla mwili wangu haujakamilika.
Siku zangu zote ulizonipangia
ziliandikwa katika kitabu chako
kabla haijakuwapo hata moja.
17Tazama jinsi gani yalivyo ya thamani
mawazo yako kwangu, Ee Mungu!
Jinsi gani jumla yake ilivyo kubwa!
18Kama ningezihesabu,
zingekuwa nyingi kuliko mchanga.
Niamkapo,
bado niko pamoja nawe.
19Laiti ungewachinja waovu, Ee Mungu!
Ondokeni kwangu, ninyi wamwaga damu!
20Wanazungumza juu yako wakiwa na kusudi baya,
adui zako wanatumia vibaya jina lako.
21Ee BWANA, je, nisiwachukie wanaokuchukia?
Nisiwachukie sana wanaoinuka dhidi yako?
22Sina kitu zaidi ya chuki dhidi yao,
ninawahesabu ni adui zangu.
23Ee Mungu, nichunguze, uujue moyo wangu,
nijaribu na ujue mawazo yangu.
24Uone kama kuna njia iletayo machukizo ndani yangu,
uniongoze katika njia ya milele.
Copyright information for Neno