Psalms 141

Maombi Ya Kuhifadhiwa Dhidi Ya Uovu

(Zaburi Ya Daudi)

Ee BWANA, ninakuita wewe,
uje kwangu hima.
Sikia sauti yangu ninapokuita.
Maombi yangu na yafike mbele zako
kama uvumba;
kuinua mikono yangu juu
na kuwe kama dhabihu ya jioni.
Ee BWANA, weka mlinzi kinywani mwangu,
weka ulinzi mlangoni mwa midomo yangu.
Usiuache moyo wangu uvutwe katika lililo baya,
nisije nikashiriki katika matendo maovu
pamoja na watu watendao mabaya,
wala nisije nikala vyakula vyao vya anasa.
Mtu mwenye haki na anipige:
ni jambo la huruma;
na anikemee,
ni mafuta kichwani mwangu.
Kichwa changu hakitalikataa.
Hata hivyo, maombi yangu daima
ni kinyume cha watenda mabaya,
watawala wao watatupwa chini
kutoka kwenye majabali,
waovu watajifunza kwamba maneno yangu
yalikuwa kweli.
Watasema, “Kama mtu anavyolima
na kuvunja ardhi,
ndivyo mifupa yetu imetawanywa
kwenye mlango wa kaburi.”
Lakini nimekaza macho yangu kwako,
Ee BWANA Mwenyezi,
ndani yako nimekimbilia,
usiniache nife.
Niepushe na mitego waliyonitegea,
kutokana na mitego
iliyotegwa na watenda mabaya.
10 Waovu na waanguke kwenye nyavu zao wenyewe,
wakati mimi ninapita salama.
Copyright information for Neno