Psalms 20

Maombi Kwa Ajili Ya Ushindi

(Kwa Mwimbishaji: Zaburi Ya Daudi)

1BWANA na akujibu unapokuwa katika dhiki,
jina la Mungu wa Yakobo na liwe kinga yako.
2Na akutumie msaada kutoka patakatifu
na akupatie msaada kutoka Sayuni.
3Na azikumbuke dhabihu zako zote
na azikubali sadaka zako za kuteketezwa.
4Na akujalie haja ya moyo wako
na aifanikishe mipango yako yote.
5Tutashangilia kwa furaha utakaposhinda,
tutainua bendera zetu kwa jina la Mungu wetu.
BWANA na akupe haja zako zote.
6Sasa nafahamu kuwa BWANA
humwokoa mpakwa mafuta wake,
humjibu kutoka mbingu yake takatifu
kwa nguvu za wokovu wa mkono wake wa kuume.
7Wengine wanatumaini magari ya vita na wengine farasi,
bali sisi tutalitumainia jina la BWANA, Mungu wetu.
8Wao wameshushwa chini na kuanguka,
bali sisi tunainuka
na kusimama imara.
9Ee BWANA, mwokoe mfalme!
Utujibu wakati tunapokuita!
Copyright information for Neno