Psalms 25

25:0 Zaburi hii imetungwa kila mstari ukianzia na herufi ya alfabeti ya Kiebrania zikifuatana tangu Aleph (A) hadi Taw (T); zote ni 22

Kumwomba Mungu Uongozi Na Ulinzi

(Zaburi Ya Daudi)

1Kwako wewe, Ee BWANA,
nainua nafsi yangu,
2ni wewe ninayekutumainia,
Ee Mungu wangu.
Usiniache niaibike,
wala usiache adui zangu wakanishinda.
3Kamwe hakuna hata mmoja anayekutegemea
atakayeaibishwa,
bali wataaibishwa wafanyao hila
bila sababu.
4Nionyeshe njia zako, Ee BWANA,
nifundishe mapito yako,
5niongoze katika kweli yako na kunifundisha,
kwa maana wewe ni Mungu Mwokozi wangu,
nalo tumaini langu liko kwako wakati wote.
6Kumbuka, Ee BWANA,
rehema zako kuu na upendo,
kwa maana zimekuwapo tangu zamani.
7Usizikumbuke dhambi za ujana wangu
wala njia zangu za uasi,
sawasawa na upendo wako unikumbuke,
kwa maana wewe ni mwema, Ee BWANA.
8BWANA ni mwema na mwenye adili,
kwa hiyo huwafundisha wenye dhambi njia zake.
9Huwaongoza wanyenyekevu katika haki,
naye huwafundisha njia yake.
10Njia zote za BWANA ni za upendo na aminifu
kwa wale wanaoshika Agano na shuhuda zake.
11Ee BWANA, kwa ajili ya jina lako,
unisamehe uovu wangu, ijapokuwa ni mwingi.
12Ni nani basi, mtu yule anayemcha BWANA?
Atamfundisha katika njia
atakayoichagua kwa ajili yake.
13Mtu huyo atafanikiwa maishani mwake,
nao wazao wake watairithi nchi.
14Siri ya BWANA iko kwa wale wamchao,
yeye huwajulisha Agano lake.
15Macho yangu humwelekea BWANA daima,
kwa kuwa yeye peke yake ndiye ataitoa
miguu yangu kutoka katika mtego.
16Nigeukie na unihurumie, kwa maana mimi
ni mpweke na mwenye kuteseka.
17Shida za moyo wangu zimeongezeka,
niokoe kutoka katika dhiki yangu.
18Uangalie mateso na shida zangu
na uniondolee dhambi zangu zote.
19Tazama adui zangu walivyo wengi,
pia uone jinsi wanavyonichukia vikali!
20Uyalinde maisha yangu na uniokoe,
usiniache niaibike,
kwa maana nimekukimbilia wewe.
21Uadilifu na uaminifu vinilinde,
kwa sababu tumaini langu ni kwako.
22Ee Mungu, mkomboe Israeli,
kutoka katika shida zake zote!
Copyright information for Neno