Psalms 26

Maombi Ya Mtu Mwema

(Zaburi Ya Daudi)

Ee BWANA, unithibitishe katika haki,
maana nimeishi maisha yasiyo na lawama;
nimetumainia BWANA
bila kusitasita.
Ee BWANA, unijaribu, unipime,
uuchunguze moyo wangu
na mawazo yangu;
kwa maana upendo wako
uko mbele yangu daima,
nami natembea siku zote
katika kweli yako.
Siketi pamoja na watu wadanganyifu,
wala siandamani na wanafiki,
ninachukia kusanyiko la watenda mabaya
na ninakataa kuketi pamoja na waovu.
Ninanawa mikono yangu kuonyesha kuwa sina hatia
na kuikaribia madhabahu yako, Ee BWANA,
nikitangaza sifa yako kwa sauti kubwa
huku nikisimulia matendo yako ya ajabu.
Ee BWANA, naipenda nyumba yako mahali unakoishi,
mahali ambapo utukufu wako hukaa.
Usiiondoe nafsi yangu pamoja na watenda dhambi,
uhai wangu pamoja na wamwaga damu,
10 ambao mikononi mwao kuna mipango miovu,
ambao mikono yao ya kuume imejaa rushwa.
11 Bali mimi ninaishi maisha yasiyo na lawama,
unikomboe na unihurumie.
12 Miguu yangu imesimama katika uwanja tambarare;
katika kusanyiko kuu nitamsifu BWANA.
Copyright information for Neno