Psalms 31

Maombi na Sifa Kwa Kuokolewa Kutoka Kwa Adui

(Zaburi Ya Daudi)

Ee BWANA, ninakukimbilia wewe,
usiache nikaaibika kamwe,
kwa haki yako uniokoe.
Nitegee sikio lako, uje uniokoe haraka,
uwe kwangu mwamba wa kimbilio,
ngome imara ya kuniokoa.
Kwa kuwa wewe ni mwamba wangu
na ngome yangu, uniongoze na kunilinda
kwa ajili ya jina lako.
Uniepushe na mtego niliotegewa,
maana wewe ndiwe kimbilio langu.
Ninaikabidhi roho yangu mikononi mwako,
Ee BWANA unikomboe,
wewe uliye Mungu wa kweli.
Ninawachukia wale wanaong'ang'ania sanamu batili;
mimi ninamtumaini BWANA.
Nitafurahia na kushangilia upendo wako,
kwa kuwa uliona mateso yangu
na ulijua maumivu ya nafsi yangu.
Hukunikabidhi kwa adui yangu
bali umeiweka miguu yangu
mahali penye nafasi.
Ee BWANA unihurumie, kwa kuwa niko kwenye shida;
macho yangu yanafifia kwa huzuni,
nafsi yangu na mwili wangu kwa sikitiko.
10 Maisha yangu yamedhoofika kwa majonzi,
naam, miaka yangu kwa kulia kwa maumivu makali;
nguvu zangu zinaisha kwa ajili ya mateso,
na mifupa yangu inachakaa.
11 Kwa sababu ya adui zangu wote,
nimedharauliwa kabisa na jirani zangu,
hata rafiki zangu wananiogopa,
wale wanionao barabarani hunikimbia.
12 Nimesahaulika miongoni mwao kama mtu aliyekufa,
nimekuwa kama chombo cha mfinyanzi kilichovunjika.
13 Kwa maana nimesikia maneno
niliyosingiziwa na watu wengi;
vitisho viko pande zote;
kwa kuwa wamefanya mashauri ya pamoja dhidi yangu
na kula njama kuniua.
14 Lakini mimi ninakutumaini wewe peke yako, Ee BWANA;
nimesema, “Wewe ndiwe Mungu wangu.”
15 Siku za maisha yangu ziko mikononi mwako,
uniokoe mikononi mwa adui zangu
na wale wanifuatiao.
16 Mwangazie mtumishi wako uso wako,
uniokoe kwa ajili ya upendo wako usiokoma.
17 Usiniache niaibike, Ee BWANA,
kwa maana nimekulilia wewe,
bali waovu waaibishwe
na kunyamazishwa Kuzimu.
18 Midomo yao isemayo uongo na inyamazishwe,
kwa maana kwa kiburi na dharau husema
kwa majivuno dhidi ya wenye haki.
19 Tazama jinsi ulivyo mkuu wema wako,
uliowawekea akiba wakuchao,
ambao huwapa wale wakukimbiliao
machoni pa watu.
20 Unawahifadhi katika uvuli wa uwepo wako
kutokana na hila za wanadamu;
katika makao yako huwaweka salama
kutokana na ndimi za mashtaka.
21 Atukuzwe BWANA,
kwa kuwa amenionyesha upendo wake wa ajabu
nilipokuwa katika mji uliozingirwa.
22 Kwa haraka yangu nilisema,
“Nimekatiliwa mbali na macho yako!”
Hata hivyo ulisikia kilio changu
ukanihurumia nilipokuita unisaidie.
23 Mpendeni BWANA ninyi watakatifu wake wote!
BWANA huwahifadhi waaminifu,
lakini wenye kiburi huwalipiza kikamilifu.
24 Iweni hodari na mjipe moyo,
ninyi nyote mnaomtumaini BWANA.
Copyright information for Neno