Psalms 35

Kuomba Msaada: Kuokolewa Kutokana Na Maadui

(Zaburi Ya Daudi)

1Ee BWANA, pingana na wale wanaopingana nami,
upigane na hao wanaopigana nami.
2Uchukue ngao na kigao,
inuka unisaidie.
3Inua mkuki wako na fumo
35.3 Fumo ni sawa na sagai, maana yake ni mkuki mfupi
lako
dhidi ya hao wanaonifuatia.
Uiambie nafsi yangu,
“Mimi ni wokovu wako.”
4Wafedheheshwe na waaibishwe
wale wanaotafuta uhai wangu,
wanaofanya shauri kuniangamiza
warudishwe nyuma kwa hofu.
5Wawe kama makapi yapeperushwayo na upepo,
malaika wa BWANA akiwafukuza;
6njia yao na iwe giza na ya utelezi,
malaika wa BWANA akiwafuatilia.
7Kwa vile walinifichia wavu wao bila sababu,
na bila sababu wamenichimbia shimo,
8maafa na yawapate ghafula:
wavu walionifichia na uwatege wenyewe,
na waanguke katika shimo hilo,
kwa maangamizo yao.
9Ndipo nafsi yangu itashangilia katika BWANA
na kuufurahia wokovu wake.
10Nitapaza sauti yangu nikisema,
“Ni nani aliye kama wewe, Ee BWANA?
Huwaokoa maskini kutokana na watu
walio na nguvu kuliko wao,
maskini na mhitaji kutokana
na wanaowanyang'anya!”
11Mashahidi wakatili wanainuka,
wananiuliza kwa mambo nisiyoyajua.
12Wananilipa baya kwa jema
na kuiacha nafsi yangu ukiwa.
13Lakini walipokuwa wagonjwa,
nilivaa nguo ya gunia
na nikajinyenyekesha kwa kufunga.
Maombi yangu yaliponirudia bila kujibiwa,
14niliendelea kuomboleza
kama vile wao ni rafiki au ndugu.
Niliinamisha kichwa chini kwa huzuni
kama vile ninayemwombolezea mama yangu.
15Lakini nilipojikwaa,
walikusanyika kwa shangwe;
washambuliaji walijikusanya dhidi yangu
bila mimi kujua.
Walinisingizia pasipo kukoma.
16Kama watu wasiomcha Mungu wamedhihaki,
wamenisagia meno.
17Ee BWANA, utatazama mpaka lini?
Niokoe maisha yangu na maangamizi yao,
uhai wangu wa thamani
kutokana na simba hawa.
18Nami nitakushukuru mbele ya kusanyiko kubwa,
nitakusifu katikati ya watu wengi.
19Usiwaache wale wanaonisimanga,
wale ambao ni adui zangu bila sababu;
usiwaache wale ambao ni adui zangu bila sababu
wakonyeze jicho kwa hila.
20Hawazungumzi kwa amani,
bali wanatunga mashtaka ya uongo
dhidi ya wale wanaoishi kwa utulivu katika nchi.
21Hunifumbulia vinywa vyao wakisema,
“Aha! Aha! Kwa macho yetu wenyewe tumeliona.”
22Ee BWANA, umeona hili, usiwe kimya.
Usiwe mbali nami, Ee BWANA.
23Amka, inuka unitetee!
Unipiganie Mungu wangu na Bwana wangu.
24Nihukumu kwa haki yako, Ee BWANA Mungu wangu,
sawasawa na haki yako;
usiwaache wakusimange.
25Usiwaache wafikiri, “Aha, hili ndilo tulilotaka!”
Au waseme, “Tumemmeza.”
26Wote wanaofurahia dhiki yangu
na waaibishwe na wachanganyikiwe;
hao wanaojiinua dhidi yangu
na wavikwe aibu na dharau.
27Wale wanaofurahia hukumu yangu ya haki
na wapige kelele za shangwe na furaha;
hebu waseme siku zote,
“BWANA atukuzwe,
ambaye amefurahia
mafanikio ya mtumishi wake.”
28Ulimi wangu utanena haki yako
na sifa zako mchana kutwa.
Copyright information for Neno