Psalms 38

Maombi Ya Mtu Anayeteseka

(Zaburi Ya Daudi)

Ee BWANA, usinikemee katika hasira yako
wala kuniadhibu katika ghadhabu yako.
Kwa kuwa mishale yako imenichoma,
na mkono wako umenishukia.
Hakuna afya mwilini mwangu
kwa sababu ya ghadhabu yako,
mifupa yangu haina uzima
kwa sababu ya dhambi zangu.
Maovu yangu yamenifunika
kama mzigo usiochukulika.
Majeraha yangu yameoza na yananuka,
kwa sababu ya upumbavu wa dhambi zangu.
Nimeinamishwa chini na kushushwa sana,
mchana kutwa nazunguka nikiomboleza.
Viuno vyangu vimejaa maumivu yaunguzayo,
hakuna afya mwilini mwangu.
Nimedhoofika na kupondwa kabisa,
nasononeka kwa maumivu makuu ya moyoni.
Ee BWANA, yote ninayoyaonea shauku
yako wazi mbele zako,
kutamani kwangu sana
hakufichiki mbele zako.
10 Moyo wangu unapigapiga,
nguvu zangu zimeniishia;
hata macho yangu yametiwa giza.
11 Rafiki na wenzangu wananikwepa
kwa sababu ya majeraha yangu;
majirani zangu wanakaa mbali nami.
12 Wale wanaotafuta uhai wangu
wanatega mitego yao,
wale ambao wangetaka kunidhuru
huongea juu ya maangamizi yangu;
hufanya shauri la hila mchana kutwa.
13 Mimi ni kama mtu kiziwi, asiyeweza kusikia,
ni kama bubu, asiyeweza kufungua kinywa chake,
14 nimekuwa kama mtu asiyesikia,
ambaye kinywa chake hakiwezi kutoa jibu.
15 Ee BWANA, ninakungojea wewe,
Ee Bwana Mungu wangu, utajibu.
16 Kwa kuwa nilisema, “Usiwaache wafurahie,
wala wasijitukuze juu yangu
mguu wangu unapoteleza.”
17 Kwa maana ninakaribia kuanguka,
na maumivu yangu yananiandama siku zote.
18 Naungama uovu wangu,
ninataabishwa na dhambi yangu.
19 Wengi ni wale ambao ni adui zangu hodari,
wale wanaonichukia bila sababu ni wengi.
20 Wanaolipa maovu kwa wema wangu
hunisingizia ninapofuata lililo jema.
21 Ee BWANA, usiniache,
usiwe mbali nami, Ee Mungu wangu.
22 Ee Bwana Mwokozi wangu,
uje upesi kunisaidia.
Copyright information for Neno