Psalms 4

Sala Ya Jioni Ya Kuomba Msaada

(Kwa Mwimbishaji: Kwa Ala Za Nyuzi Za Muziki. Zaburi Ya Daudi)

Unijibu nikuitapo,
Ee Mungu wangu mwenye haki!
Unipumzishe katika shida zangu,
nirehemu, usikie ombi langu.
Enyi watu, mtabadilisha utukufu wangu
kuwa aibu mpaka lini?
Mtapenda udanganyifu
na kufuata miungu ya uongo mpaka lini?
Fahamuni hakika kwamba BWANA amewatenga
wale wamchao kwa ajili yake;
BWANA atanisikia nimwitapo.
Katika hasira yako usitende dhambi,
mkiwa vitandani mwenu, mtulie kimya
mkiichunguza mioyo yenu.
Toeni dhabihu iliyo sahihi
na mumtegemee BWANA.
Wengi wanauliza, “Ni nani awezaye
kutuonyesha jema lo lote?”
Ee BWANA, utuangazie nuru ya uso wako.
Wewe umejaza moyo wangu kwa furaha kubwa
kuliko watu waliopata ngano na divai kwa wingi.
Nitajilaza chini na kulala kwa amani,
kwa kuwa wewe peke yako, Ee BWANA,
waniwezesha kukaa kwa salama.
Copyright information for Neno