Psalms 45

Wimbo Wa Arusi Ya Kifalme

(Kwa Mwimbishaji: Utenzi Wa Wana Wa Kora)

Moyo wangu umesisimuliwa na jambo
jema ninapomsimulia mfalme mabeti yangu,
ulimi wangu ni kalamu ya mwandishi stadi.
Wewe ni bora kuliko watu wengine wote
na midomo yako imepakwa neema,
kwa kuwa Mungu amekubariki milele.
Jifunge upanga wako pajani mwako, Ee mwenye nguvu,
jivike fahari na utukufu.
Katika fahari yako songa mbele kwa ushindi,
kwa ajili ya kweli, unyenyekevu na haki,
mkono wako wa kuume na uonyeshe matendo ya kutisha.
Mishale yako mikali na ichome mioyo ya adui za mfalme,
mataifa na yaanguke chini ya nyayo zako.
Ee Mungu, kiti chako cha enzi
kitadumu milele na milele,
fimbo ya utawala wa haki
itakuwa fimbo ya utawala wa ufalme wako.
Unaipenda haki na kuchukia uovu;
kwa hiyo Mungu, Mungu wako,
amekuweka juu ya rafiki zako,
kwa kukupaka mafuta ya furaha.
Mavazi yako yote ni yenye harufu nzuri
ya manemane, udi na mdalasini;
kutoka kwenye majumba ya kifalme
yaliyopambwa kwa pembe za ndovu,
sauti za vinanda vya nyuzi
zinakufanya ufurahi.
Binti za wafalme ni miongoni mwa wanawake wako waheshimiwa;
kuume kwako yupo bibi arusi wa kifalme
aliyevaa dhahabu ya Ofiri.
10 Sikiliza, ewe binti, fikiri na utege sikio:
Sahau watu wako na wa nyumbani mwa baba yako.
11 Mfalme ameshangazwa na uzuri wako;
mheshimu, kwa kuwa yeye ni bwana wako.
12 Binti wa Tiro atakuletea zawadi,
watu wenye utajiri watatafuta upendeleo wako.
13 Utukufu wote ni binti mfalme katika chumba chake;
vazi lake limefumwa kwa kuchanganya nyuzi za dhahabu.
14 Akiwa amevalia mavazi yaliyotariziwa anaongozwa kwa mfalme,
mabikira wenzake wanamfuata
na wanaletwa kwako.
15 Wanaingizwa ndani kwa shangwe na furaha,
na kuingia katika jumba la mfalme.
16 Wana wenu watachukua nafasi za baba zenu,
mtawafanya wana wa kifalme katika nchi yote.
17 Nitadumisha kumbukumbu lako katika vizazi vyote,
kwa hiyo mataifa watakusifu milele na milele.
Copyright information for Neno