Psalms 47

Mtawala Mwenye Enzi Yote

(Kwa Mwimbishaji: Zaburi Ya Wana Wa Kora)

Pigeni makofi, enyi mataifa yote,
mpigieni Mungu kelele za shangwe!
Jinsi gani alivyo wa kutisha, BWANA Aliye Juu Sana,
Mfalme mkuu juu ya dunia yote.
Ametiisha mataifa chini yetu
na mataifa chini ya miguu yetu.
Alituchagulia urithi wetu kwa ajili yetu
fahari ya Yakobo, aliyempenda.
Mungu amepaa katikati ya kelele za shangwe,
BWANA katikati ya sauti za tarumbeta.
Mwimbieni Mungu sifa, imbeni sifa,
mwimbieni sifa Mfalme wetu, imbeni sifa.
Kwa kuwa Mungu ni mfalme wa dunia yote,
mwimbieni zaburi za sifa.
Mungu anatawala juu ya mataifa,
Mungu ameketi juu ya kiti chake cha enzi kitakatifu.
Wakuu wa mataifa wanakusanyika kama watu wa Mungu wa Abrahamu,
kwa kuwa wafalme wa dunia ni mali ya Mungu;
yeye ametukuka sana.
Copyright information for Neno