Psalms 53

Uovu Wa Wanadamu

(Zab 14)

(Kwa Mwimbishaji: Mtindo Wa Mahalathi. Utenzi Wa Daudi)

1Mpumbavu anasema moyoni mwake,
“Hakuna Mungu.”
Wameharibika, na njia zao ni za uovu kabisa,
hakuna hata mmoja atendaye mema.
2Mungu huwachungulia wanadamu chini
kutoka mbinguni
aone kama wako wenye akili,
wo wote wanaomtafuta Mungu.
3Kila mmoja amegeukia mbali,
wameharibika wote pamoja,
hakuna hata mmoja atendaye mema,
naam! Hata mmoja.
4Je, watendao mabaya kamwe hawatajifunza,
wale ambao huwala watu wangu
kama watu walavyo mkate,
na ambao hawamwiti Mungu?
5Hapo watatetemeka kwa hofu kuu,
ambapo hakuna cha kutetemesha.
Mungu alitawanya mifupa ya wale waliokushambulia;
umewaaibisha, kwa sababu Mungu amewadharau.
6Laiti wokovu wa Israeli ungalikuja kutoka Sayuni!
Wakati Mungu arejeshapo wafungwa wa watu wake,
Yakobo na ashangilie, Israeli na afurahi!
Copyright information for Neno