Psalms 61

Kuomba Ulinzi

(Kwa Mwimbishaji: Kwa Ala Za Nyuzi Za Uimbaji. Zaburi Ya Daudi)

1Ee Mungu, sikia kilio changu,
usikilize maombi yangu.
2Kutoka miisho ya dunia ninakuita,
ninaita huku moyo wangu unadhoofika;
uniongoze kwenye mwamba
ule ulio juu kuliko mimi.
3Kwa kuwa umekuwa kimbilio langu,
ngome imara dhidi ya adui.
4Natamani kukaa hemani mwako milele
na kupata kimbilio chini ya uvuli wa mbawa zako.
5Ee Mungu, kwa kuwa umesikia nadhiri zangu,
umenipa urithi wa wale wanaoliogopa jina lako.
6Mwongezee mfalme siku za maisha yake,
miaka yake kwa vizazi vingi.
7Yeye na atawazwe kwenye kiti cha enzi
mbele za Mungu milele;
amuru upendo wako na uaminifu wako vimlinde.
8Ndipo daima nitaliimbia sifa jina lako
na kuzitimiza nadhiri zangu siku baada ya siku.
Copyright information for Neno