Psalms 65

Kusifu Na Kushukuru

(Kwa Mwimbishaji: Zaburi Ya Daudi. Wimbo)

Ee Mungu, sifa zakungojea katika Sayuni;
kwako wewe nadhiri zetu zitatimizwa.
Ee wewe usikiaye maombi,
kwako wewe watu wote watakuja.
Tulipokuwa tumefunikwa kabisa na dhambi,
wewe ulisamehe makosa yetu.
Heri wale uliowachagua
na kuwaleta karibu ili waishi katika nyua zako!
Tunashibishwa kwa mema ya nyumba yako,
mema ya Hekalu lako takatifu.
Unatujibu kwa matendo ya kushangaza ya haki,
Ee Mungu Mwokozi wetu,
tumaini la miisho yote ya duniani
na la bahari zilizo mbali sana,
uliyeumba milima kwa uwezo wako,
ukiwa umejivika nguvu,
uliyenyamazisha dhoruba za bahari,
ngurumo za mawimbi yake,
na ghasia za mataifa.
Wale wanaoishi mbali sana
wanaogopa maajabu yako,
kule asubuhi ipambazukiapo
na kule jioni inakofifilia
umeziita nyimbo za furaha.
Waitunza nchi na kuinyeshea,
waitajirisha kwa wingi.
Vijito vya Mungu vimejaa maji
ili kuwapa watu nafaka,
kwa maana wewe umeviamuru.
10 Umeilowesha mifereji yake
na kusawazisha kingo zake;
umeilainisha kwa manyunyu
na kuibariki mimea yake.
11 Umeuvika mwaka taji ya baraka,
magari yako yanafurika kwa wingi.
12 Mbuga za majani za jangwani umezineemesha;
vilima vimevikwa furaha.
13 Penye nyanda za malisho pamejaa makundi ya wanyama,
na mabonde yamepambwa kwa mavuno;
vyote vinashangilia kwa furaha na kuimba.
Copyright information for Neno