Psalms 8

Utukufu Wa Mungu Na Heshima Ya Mwanadamu

(Kwa Mwimbishaji: Mtindo Wa Gitithi. Zaburi Ya Daudi)

Ee BWANA, Bwana wetu,
tazama jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote!
Umeuweka utukufu wako
juu ya mbingu.
Midomoni mwa watoto wachanga na wanyonyao
umeweka sifa,
kwa sababu ya watesi wako,
kuwanyamazisha adui na mlipiza kisasi.
Nikiziangalia mbingu zako,
kazi ya vidole vyako,
mwezi na nyota,
ulizoziratibisha,
mwanadamu ni kitu gani hata umkumbuke,
binadamu hata umwangalie?
Umemfanya mdogo punde kuliko Mungu,
umemvika taji ya utukufu na heshima.
Umemfanya mtawala juu ya kazi za mikono yako;
umevitia vitu vyote chini ya miguu yake.
Kondoo, mbuzi na ng'ombe wote pia,
naam, na wanyama wa kondeni,
ndege wa angani na samaki wa baharini,
naam, kila kiogeleacho katika njia za bahari.
Ee BWANA, Bwana wetu,
tazama jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote!
Copyright information for Neno