Psalms 98

Mungu Mtawala Wa Dunia

Mwimbieni BWANA wimbo mpya,
kwa maana ametenda mambo ya ajabu;
kitanga chake cha kuume na mkono wake mtakatifu
umemfanyia wokovu.
BWANA ameufanya wokovu wake ujulikane
na amedhihirisha haki yake kwa mataifa.
Ameukumbuka upendo wake
na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli;
miisho yote ya dunia imeuona
wokovu wa Mungu wetu.
Mpigieni kelele za shangwe, dunia yote,
ipaze sauti kwa nyimbo za shangwe na vinanda;
mwimbieni BWANA kwa kinubi,
kwa kinubi na sauti za kuimba,
kwa tarumbeta na mvumo wa baragumu
za pembe za kondoo dume:
shangilieni kwa furaha mbele za BWANA,
aliye Mfalme.
Bahari na ivume na kila kiliomo ndani yake,
dunia na wote wakaao ndani yake.
Mito na ipige makofi,
milima na iimbe pamoja kwa furaha,
vyote na viimbe mbele za BWANA,
kwa maana yuaja kuhukumu dunia.
Atahukumu dunia kwa haki
na mataifa kwa haki.
Copyright information for Neno