Revelation of John 5

Kitabu Na Mwana-Kondoo

1Kisha nikaona katika mkono wake wa kuume yule aliyeketi kwenye kile kiti cha enzi, kitabu kilichoandikwa ndani na upande wa nyuma kikiwa kimefungwa kwa lakiri saba. 2Nami nikamwona malaika mwenye nguvu akitangaza kwa sauti kuu, akisema, “Ni nani anayestahili kuzivunja hizo lakiri na kukifungua hicho kitabu?” 3Lakini hapakuwa na ye yote mbinguni wala duniani au chini ya dunia aliyeweza kukifungua hicho kitabu wala hata kutazama ndani yake. 4Nikalia sana sana kwa sababu hakuonekana ye yote anayestahili kukifungua hicho kitabu wala kutazama ndani yake. 5Kisha, mmoja wa wale wazee akaniambia, “Usilie! Tazama, Simba wa kabila la Yuda, wa Uzao wa Daudi, ameshinda. Yeye ndiye anayeweza kukifungua hicho kitabu na kuvunja hizo lakiri zake saba.”

6Ndipo nikaona katikati ya kile kiti cha enzi na wale viumbe wenye uhai wanne na miongoni mwa wale wazee, Mwana-Kondoo amesimama, akiwa kama amechinjwa. Alikuwa na pembe saba na macho saba, ambazo ndizo zile Roho saba
5.6 Roho saba za Mungu hapa inamaanisha Roho wa Mungu katika ukamilifu wa utendaji wake
za Mungu zilizotumwa duniani pote.
7Huyo Mwana-Kondoo akaja na kukitwaa kile kitabu kutoka kwenye mkono wa kuume wa yule aliyeketi kwenye kile kiti cha enzi. 8Alipokwisha kukitwaa kile kitabu, wale viumbe wenye uhai wanne pamoja na wale wazee ishirini na wanne wakaanguka mbele ya yule Mwana-Kondoo. Kila mmoja wao alikuwa na kinubi, nao walikuwa wameshika mabakuli ya dhahabu yaliyojaa uvumba, ambayo ni maombi ya watakatifu. 9Nao wakaimba wimbo mpya, wakisema: “Wewe unastahili kukitwaa kitabu
na kuzivunja lakiri zake,
kwa sababu ulichinjwa
na kwa damu yako ukamnunulia Mungu watu
kutoka katika kila kabila, kila lugha,
kila jamaa na kila taifa.
10Wewe umewafanya hawa wawe ufalme na makuhani
wa kumtumikia Mungu wetu,
nao watatawala duniani.”11Kisha nikatazama, nikasikia sauti za malaika wengi wakiwa wamekizunguka kile kiti cha enzi, pamoja na wale viumbe wenye uhai wanne na wale wazee ishirini na wanne, idadi yao ilikuwa kumi elfu mara kumi elfu na maelfu ya maelfu. 12Nao wakiimba kwa sauti kuu, wakisema: “Anastahili Mwana-Kondoo, yeye aliyechinjwa,
kupokea uweza na utajiri na hekima na nguvu
na heshima na utukufu na sifa!”13Kisha nikasikia kila kiumbe mbinguni na duniani, chini ya nchi na baharini na vyote vilivyomo ndani yake vikiimba: “Sifa na heshima na utukufu na uweza
ni vyake yeye aketiye juu ya hicho kiti cha enzi
na kwa Mwana-Kondoo,
milele na milele!”14Wale viumbe wenye uhai wanne wakasema, “Amen!” Nao wale wazee ishirini na wanne wakaanguka kifudifudi wakaabudu.

Copyright information for Neno