Song of Solomon 7

Ee binti wa mwana wa mfalme,
tazama jinsi inavyopendeza miguu yako katika viatu!
Miguu yako yenye madaha ni kama vito vya thamani,
kazi ya mikono ya fundi stadi.
Kitovu chako ni kama bilauri ya mviringo
ambayo kamwe haikosi divai iliyochanganywa.
Kiuno chako ni kichuguu cha ngano
kilichozungukwa kwa yungiyungi.
Matiti yako ni kama wana paa wawili,
mapacha wa swala.
Shingo yako ni kama mnara wa pembe ya ndovu.
Macho yako ni vidimbwi vya Heshboni
karibu na lango la Beth-Rabi.
Pua yako ni kama mnara wa Lebanoni
ukitazama kuelekea Dameski.
Kichwa chako kinakuvika taji kama mlima Karmeli.
Nywele zako ni kama zulia nene la kutundika ukutani;
mfalme ametekwa na mashungi yake.
Tazama jinsi ulivyo mzuri na unavyopendeza,
Ee pendo, kwa uzuri wako!
Umbo lako ni kama la mtende,
nayo matiti yako kama vishada vya matunda.
Nilisema, “Nitakwea mtende,
nami nitayashika matunda yake.”
Matiti yako na yawe kama vishada vya mzabibu,
harufu nzuri ya pumzi yako kama matofaa,
na kinywa chako kama divai
bora kuliko zote. Mpendwa
Divai na iende moja kwa moja kwa mpenzi wangu,
ikitiririka pole pole juu ya midomo na meno.
10 Mimi ni mali ya mpenzi wangu,
nayo shauku yake ni juu yangu.
11 Njoo, mpenzi wangu, twende mashambani,
twende tukalale huko vijijini.
12 Hebu na twende mapema
katika mashamba ya mizabibu
tuone kama mizabibu imechipua,
kama maua yake yamefunguka,
pia kama mikomamanga imetoa maua:
huko nitakupa penzi langu.
13 Mitunguja hutoa harufu zake nzuri,
kwenye milango yetu kuna matunda mazuri,
mapya na ya zamani,
ambayo nimekuhifadhia wewe,
mpenzi wangu.
Copyright information for Neno