1 Corinthians 7

Kuhusu Ndoa

1 aBasi kuhusu mambo yale mliyoyaandika: Ni vyema mwanaume asimguse mwanamke. 2Lakini ili kuepuka zinaa, kila mwanaume na awe na mke wake mwenyewe na kila mwanamke awe na mume wake mwenyewe. 3 bMume atimize wajibu wake wa ndoa kwa mkewe, naye vivyo hivyo mke kwa mumewe. 4Mwanamke hana mamlaka juu ya mwili wake bali mumewe, wala mume hana mamlaka juu ya mwili wake bali mkewe. 5 cMsinyimane, isipokuwa mmekubaliana kufanya hivyo kwa muda fulani ili mweze kujitoa kwa maombi, kisha mrudiane tena ili Shetani asije akapata nafasi ya kuwajaribu kwa sababu ya kutokuwa na kiasi. 6 dNasema haya kama ushauri na si amri. 7 eLaiti watu wangekuwa kama mimi nilivyo. Lakini kila mtu amepewa kipawa chake kutoka kwa Mungu, mmoja ana kipawa cha namna hii na mwingine ana cha namna ile.

8 fKwa wale wasiooa na kwa wajane, nasema hivi, ingekuwa vizuri wasioe. 9 gLakini kama hawawezi kujizuia, basi waoe na kuolewa, kwa maana ni afadhali kuoa au kuolewa kuliko kuwaka tamaa.

10 hKwa wale waliooana nawapa amri (si mimi ila ni Bwana): Mke asitengane na mumewe. 11 iLakini akitengana, ni lazima akae bila kuolewa, ama sivyo apatane tena na mumewe. Wala mume asimpe mkewe talaka.

12 jLakini kwa wengine nasema (si Bwana ila ni mimi): Kama ndugu ana mke asiyeamini, naye huyo mke anakubali kuishi pamoja naye, basi asimwache. 13Naye mwanamke aaminiye kama ameolewa na mwanaume asiyeamini na huyo mume anakubali kuishi naye, basi huyo mwanamke asimwache. 14 kKwa maana huyo mume asiyeamini anatakaswa kupitia mkewe, naye mke asiyeamini anatakaswa kupitia mumewe anayeamini. Kama isingalikuwa hivyo watoto wenu wangalikuwa si safi, lakini ilivyo sasa wao ni watakatifu. 15 lLakini kama yule asiyeamini akijitenga, basi afanye hivyo. Katika hali kama hiyo mwanamke au mwanaume aaminiye hafungwi, kwa sababu Mungu ametuita tuishi kwa amani. 16 mWewe mke, unajuaje kama utamwokoa mumeo? Au wewe mume unajuaje kama utamwokoa mkeo?

Kuishi Kama Alivyoagiza Bwana

17 nLakini kila mtu na aishi maisha aliyopangiwa na Bwana, yale Mungu aliyomwitia. Hii ni sheria ninayoiweka kwa makanisa yote. 18 oJe, mtu alikuwa tayari ametahiriwa alipoitwa? Asijifanye asiyetahiriwa. Je, mtu alikuwa hajatahiriwa alipoitwa? Asitahiriwe. 19 pKutahiriwa si kitu, na kutokutahiriwa si kitu. Lakini kuzitii amri za Mungu ndilo jambo muhimu. 20 qBasi kila mmoja wenu na abaki katika hali aliyoitwa nayo. 21Je, wewe ulipoitwa ulikuwa mtumwa? Jambo hilo lisikusumbue. Ingawaje unaweza kupata uhuru, tumia nafasi uliyo nayo sasa kuliko wakati mwingine wowote. 22 rKwa maana yeyote aliyeitwa katika Bwana akiwa mtumwa yeye ni mtu huru kwa Bwana, kama vile yeyote aliyekuwa huru alipoitwa yeye ni mtumwa wa Kristo. 23 sMlinunuliwa kwa gharama; msiwe watumwa wa wanadamu. 24Ndugu zangu, kama kila mtu alivyoitwa, akae katika wito wake alioitiwa na Mungu.

Wajane Na Wasioolewa

25 tBasi, kuhusu wale walio bikira, mimi sina amri kutoka kwa Bwana, lakini mimi natoa shauri kama mtu ambaye ni mwaminifu kwa rehema za Bwana. 26 uKwa sababu ya shida iliyoko kwa sasa, naona ni vyema mkibaki kama mlivyo. 27Je, umeolewa? Basi usitake talaka. Je, hujaoa? Usitafute mke. 28 vLakini kama ukioa, hujatenda dhambi; na kama bikira akiolewa, hajatenda dhambi. Lakini wale wanaooa watakabiliana na matatizo mengi katika maisha haya, nami nataka kuwazuilia hayo.

29 wLakini ndugu zangu, nina maana kwamba muda uliobaki ni mfupi. Tangu sasa wale waliooa waishi kama wasio na wake; 30nao wanaoomboleza, kama ambao hawaombolezi; wenye furaha kama wasiokuwa nayo; wale wanaonunua, kama vile vitu walivyonunua si mali yao; 31 xnao wale wanaoshughulika na vitu vya dunia hii, kama ambao hawahusiki navyo. Kwa maana dunia hii kama tunavyoiona sasa inapita.

32 yNingetaka msiwe na masumbufu. Mwanaume ambaye hajaoa anajishughulisha na mambo ya Bwana, jinsi ya kumpendeza Bwana. 33 zLakini mwanaume aliyeoa anajishughulisha na mambo ya dunia, jinsi ya kumfurahisha mkewe, 34 aana mawazo yake yamegawanyika. Mwanamke asiyeolewa hujishughulisha na mambo ya Bwana: lengo lake ni awe mtakatifu kimwili na kiroho. Lakini yule aliyeolewa hujishughulisha na mambo ya dunia, jinsi atakavyoweza kumfurahisha mumewe. 35 abNinasema haya kwa faida yenu wenyewe, sio ili kuwawekea vizuizi bali mpate kuishi kwa jinsi ilivyo vyema bila kuvutwa pengine katika kujitoa kwenu kwa Bwana.

36 acKama mtu yeyote anadhani kwamba hamtendei ilivyo sawa mwanamwali ambaye amemposa, naye akiwa umri wake unazidi kuendelea na mtu huyo anajisikia kwamba inampasa kuoa, afanye kama atakavyo. Yeye hatendi dhambi. Yawapasa waoane. 37Lakini mwanaume ambaye ameamua moyoni mwake kutooa bila kulazimishwa na mtu yeyote, bali anaweza kuzitawala tamaa zake kutomwoa huyo mwanamwali, basi anafanya ipasavyo. 38 adHivyo basi, mwanaume amwoaye mwanamwali afanya vyema, lakini yeye asiyemwoa afanya vyema zaidi.

39 aeMwanamke aliyeolewa amefungwa na sheria maadamu mumewe yu hai. Lakini mumewe akifa, basi mwanamke huyo yuko huru kuolewa na mume mwingine ampendaye, lakini lazima awe katika Bwana. 40 afLakini kwa maoni yangu, angekuwa na furaha zaidi akibaki alivyo. Nami nadhani pia nina Roho wa Mungu.

Copyright information for SwhNEN