1 Kings 2

Maagizo Ya Daudi Kwa Solomoni

1 aSiku zilipokaribia za Daudi kufa, akampa mwanawe Solomoni agizo.

2 bAkasema, “Mimi ninakaribia kwenda njia ya dunia yote. Hivyo uwe hodari, jionyeshe kuwa mwanaume, 3 cshika lile Bwana Mungu wako analokuagiza: Enenda katika njia zake, ushike maagizo na amri zake, sheria zake na kanuni zake, kama ilivyoandikwa katika Sheria ya Mose, ili upate kustawi katika yote ufanyayo na popote uendako, 4ili kwamba Bwana aweze kunitimizia ahadi yake: ‘Kama wazao wako wakiangalia sana wanavyoishi, na kama wakienenda kwa uaminifu mbele zangu kwa mioyo yao yote na kwa roho zao zote, kamwe hutakosa kuwa na mtu kwenye kiti cha ufalme cha Israeli.’

5 d“Sasa wewe mwenyewe unafahamu lile Yoabu mwana wa Seruya alilonitendea, lile alilofanya kwa majemadari wawili wa majeshi ya Israeli, Abneri mwana wa Neri, na Amasa mwana wa Yetheri. Aliwaua, akimwaga damu yao wakati wa amani kama vile ni kwenye vita, tena akaipaka damu ile kwenye mkanda uliokuwa kiunoni mwake na viatu alivyovaa miguuni mwake. 6Shughulika naye kwa kadiri ya hekima yako, lakini usiache kichwa chake chenye mvi kishukie kaburi kwa amani.

7“Lakini uwaonyeshe wema wana wa Barzilai wa Gileadi na uwaruhusu wawe miongoni mwa wale walao mezani pako. Walisimama nami nilipomkimbia ndugu yako Absalomu.

8“Ukumbuke, unaye Shimei mwana wa Gera, Mbenyamini kutoka Bahurimu, ambaye alinilaani kwa laana kali siku niliyokwenda Mahanaimu. Aliposhuka kunilaki huko Yordani, nilimwapia kwa Bwana: ‘Sitakuua kwa upanga!’ 9Lakini sasa, usidhani kwamba hana hatia. Wewe ni mtu wa hekima, utajua la kumtendea. Zishushe mvi zake kaburini kwa damu.”

10Kisha Daudi akapumzika pamoja na baba zake naye akazikwa katika Mji wa Daudi. 11Daudi alikuwa ametawala juu ya Israeli miaka arobaini: huko Hebroni alitawala miaka saba, na katika Yerusalemu akatawala miaka thelathini na mitatu. 12Kwa hiyo Solomoni akaketi katika kiti cha ufalme cha baba yake Daudi, nao utawala wake ukaimarika sana.

Kiti Cha Ufalme Cha Solomoni Chaimarishwa

13 eBasi Adoniya, mwana wa Hagithi, akaenda kwa Bathsheba, mama yake Solomoni. Bathsheba akamuuliza, “Je, umekuja kwa amani?”

Akajibu, “Ndiyo, kwa amani.”
14Kisha akaongeza, “Ninalo jambo la kukuambia.”

Akajibu, “Waweza kulisema.”

15Akasema, “Kama unavyojua, ufalme ulikuwa wangu. Israeli wote waliniangalia mimi kama mfalme wao. Lakini mambo yalibadilika, ufalme umekwenda kwa ndugu yangu, kwa maana umemjia kutoka kwa Bwana. 16Sasa ninalo ombi moja ninalokuomba. Usinikatalie.”

Bathsheba akasema, “Waweza kuliomba.”

17Kwa hiyo akaendelea kusema, “Tafadhali mwombe Mfalme Solomoni, anipatie Abishagi, Mshunami, awe mke wangu; hatakukatalia wewe.”

18Bathsheba akamjibu, “Vema sana, nitazungumza na mfalme kwa ajili yako.”

19Bathsheba alipokwenda kwa Mfalme Solomoni kuzungumza naye kwa ajili ya Adoniya, mfalme alisimama kumlaki mama yake, akamwinamia na kuketi kwenye kiti chake cha ufalme. Akaamuru kiti cha ufalme kuletwa kwa ajili ya mama yake mfalme, naye akaketi mkono wake wa kuume.

20 fBathsheba akamwambia mfalme, “Ninalo ombi moja dogo la kukuomba; usinikatalie.”

Mfalme akajibu, “Omba, mama yangu; sitakukatalia.”

21 gAkasema, “Mruhusu Abishagi, Mshunami, aolewe na ndugu yako Adoniya.”

22Mfalme Solomoni akamjibu mama yake, “Kwa nini uombe Abishagi, Mshunami, kwa ajili ya Adoniya? Ungeweza pia kuomba ufalme kwa ajili yake, kwani yeye ni ndugu yangu mkubwa: naam, kwa ajili yake, na kwa kuhani Abiathari na Yoabu mwana wa Seruya!”

23Mfalme Solomoni akaapa kwa Bwana, akasema: “Mungu na aniulie mbali, tena bila huruma, ikiwa Adoniya hatalipa kwa uhai wake kwa ajili ya ombi hili! 24Basi sasa, hakika kama Bwana aishivyo, yeye ambaye ameniimarisha salama kwenye kiti cha ufalme cha Daudi baba yangu, naye amenipa ufalme wa kudumu kama alivyoahidi, Adoniya atauawa leo!” 25Hivyo Mfalme Solomoni akatoa amri kwa Benaya mwana wa Yehoyada, naye akampiga Adoniya akafa.

26 hMfalme akamwambia kuhani Abiathari, “Nenda huko Anathothi katika mashamba yako. Wewe unastahili kufa, lakini sitakuua sasa, kwa sababu ulilichukua Sanduku la Bwana Mwenyezi mbele ya Daudi baba yangu na ulishiriki taabu zote za baba yangu.” 27Hivyo Solomoni akamwondoa Abiathari kwenye ukuhani wa Bwana, akilitimiza neno la Bwana alilokuwa amenena huko Shilo kuhusu nyumba ya Eli.

28 iHabari zilipomfikia Yoabu, ambaye alikuwa amefanya shauri baya na Adoniya, lakini sio na Absalomu, alikimbilia kwenye hema la Bwana na kushika pembe za madhabahu. 29Mfalme Solomoni akaambiwa kuwa Yoabu amekimbilia kwenye hema la Bwana naye alikuwa kando ya madhabahu. Basi Solomoni akamwagiza Benaya mwana wa Yehoyada: “Nenda ukamuue!”

30Ndipo Benaya akaingia kwenye hema la Bwana na kumwambia Yoabu, “Mfalme anasema, ‘Toka nje!’ ”

Lakini akajibu, “La! Nitafia hapa hapa.”

Benaya akamwarifu mfalme, “Hivi ndivyo Yoabu alivyonijibu.”

31 jKisha mfalme akamwamuru Benaya, “Fanya kama asemavyo. Muue na kumzika, ili uniondolee mimi na nyumba ya baba yangu dhambi ya damu isiyokuwa na hatia ile Yoabu aliyoimwaga. 32Bwana atamlipiza kwa ajili ya damu aliyoimwaga, kwa sababu pasipo Daudi baba yangu kujua, aliwashambulia watu wawili na kuwaua kwa upanga. Wote wawili, Abneri mwana wa Neri, jemadari wa jeshi la Israeli, na Amasa mwana wa Yetheri, jemadari wa jeshi la Yuda, walikuwa watu wazuri na wanyofu kuliko yeye. 33Hatia ya damu yao na iwe juu ya kichwa cha Yoabu na wazao wake milele. Lakini kwa Daudi na uzao wake, nyumba yake na kiti chake cha ufalme, iwepo amani ya Bwana milele.”

34 kBasi Benaya mwana wa Yehoyada akakwea, akampiga na kumuua Yoabu, naye akazikwa katika nchi yake mwenyewe katika jangwa. 35Mfalme akamweka Benaya mwana wa Yehoyada juu ya jeshi kwenye nafasi ya Yoabu na kumweka kuhani Sadoki badala ya Abiathari.

36 lKisha mfalme akatuma ujumbe kwa Shimei na kumwambia, “Ujijengee nyumba huko Yerusalemu uishi huko, lakini usiende mahali pengine popote. 37 mSiku utakayoondoka kuvuka Bonde la Kidroni, uwe na hakika utakufa; damu yako itakuwa juu ya kichwa chako mwenyewe.”

38 nShimei akamjibu mfalme, “Ulilolisema ni jema. Mtumishi wako atatenda kama bwana wangu mfalme alivyosema.” Naye Shimei akakaa Yerusalemu kwa muda mrefu.

39 oLakini baada ya miaka mitatu, watumwa wawili wa Shimei wakatoroka kwenda kwa Akishi mwana wa Maaka, mfalme wa Gathi, naye Shimei akaambiwa, “Watumwa wako wako Gathi.” 40 pKwa ajili ya hili, Shimei akatandika punda wake, akaenda kwa Akishi huko Gathi kuwatafuta watumwa wake. Basi Shimei akaondoka na kuwarudisha watumwa wake kutoka Gathi.

41 qSolomoni alipoambiwa kuwa Shimei ametoka Yerusalemu na kwenda Gathi na amekwisha kurudi, 42 rmfalme akamwita Shimei na kumwambia, “Je, sikukuapiza kwa Bwana na kukuonya kuwa, ‘Siku utakayoondoka kwenda mahali pengine popote, uwe na hakika utakufa?’ Wakati ule uliniambia, ‘Ulilolisema ni jema. Nitatii!’ 43 sKwa nini basi hukutunza kiapo chako kwa Bwana na kutii amri niliyokupa?”

44Pia mfalme akamwambia Shimei, “Unajua katika moyo wako makosa uliyomtendea baba yangu Daudi. Sasa Bwana atakulipiza kwa ajili ya mabaya yako uliyotenda. 45Lakini Mfalme Solomoni atabarikiwa, na kiti cha ufalme cha Daudi kitakuwa imara mbele za Bwana milele.”

46Kisha mfalme akatoa amri kwa Benaya mwana wa Yehoyada, naye akatoka nje, akampiga Shimei na kumuua.

Sasa ufalme ukawa umeimarika kikamilifu mikononi mwa Solomoni.

Copyright information for SwhNEN