1 Thessalonians 2

Huduma Ya Paulo Huko Thesalonike

1 aNdugu zangu, kwa kuwa ninyi wenyewe mnajua ya kwamba kuja kwetu kwenu hakukuwa bure, 2 bkama vile mjuavyo, tulikuwa tumeteswa na kutukanwa huko Filipi, lakini hata hivyo, kwa msaada wa Mungu wetu, tulikuwa na ujasiri wa kuwaambia Injili ya Mungu ingawa kulikuwa na upinzani mkubwa. 3 cKwa maana himizo letu halikutokana na hila wala nia mbaya au udanganyifu. 4 dKinyume chake, tulinena kama watu tuliokubaliwa na Mungu tukakabidhiwa Injili. Sisi hatujaribu kuwapendeza wanadamu bali kumpendeza Mungu, yeye ayachunguzaye mawazo ya ndani sana ya mioyo yetu. 5 eKama mjuavyo, hatukuja kwenu kwa maneno ya kujipendekeza au maneno yasiyo ya kweli ili kuficha tamaa mbaya: Mungu ndiye shahidi yetu. 6 fWala hatukuwa tunatafuta sifa kutoka kwa wanadamu, wala kutoka kwenu au kwa mtu mwingine awaye yote.

Kama mitume wa Kristo tungaliweza kuwa mzigo kwenu,
7 glakini tulikuwa wapole katikati yenu, kama mama anayewatunza watoto wake wadogo. 8 hTuliwapenda sana kiasi kwamba tulifurahia kushirikiana nanyi, si Injili ya Mungu tu, bali hata maisha yetu, kwa sababu mlikuwa wa thamani mno kwetu. 9 iNdugu zetu, mnakumbuka juhudi yetu na taabu yetu. Tulifanya kazi usiku na mchana, ili tusimlemee mtu yeyote wa kwenu wakati tulipokuwa tunawahubiria Injili ya Mungu.

10 jNinyi wenyewe ni mashahidi na Mungu pia, jinsi tulivyokuwa watakatifu, wenye haki na wasio na lawama miongoni mwenu ninyi mlioamini. 11 kMaana mnajua kwamba tuliwatendea kila mmoja wenu kama vile baba awatendeavyo watoto wake. 12 lTuliwatia moyo, tuliwafariji na kuwahimiza kuishi maisha yampendezayo Mungu, anayewaita katika Ufalme na utukufu wake.

13 mNasi pia tunamshukuru Mungu bila kukoma kwa sababu mlipolipokea neno la Mungu mlilosikia kutoka kwetu, hamkulipokea kama neno la wanadamu, bali mlilipokea kama lilivyo hasa, neno la Mungu, litendalo kazi ndani yenu ninyi mnaoamini. 14 nKwa maana ninyi ndugu zetu, mlifanyika wafuasi wa makanisa ya Mungu yaliyoko ndani ya Kristo Yesu katika Uyahudi. Mlipata mateso yale yale kutoka kwa watu wenu wenyewe kama vile makanisa hayo yalivyoteswa na Wayahudi, 15 owale waliomuua Bwana Yesu na manabii, nasi wakatufukuza pia. Watu hao walimchukiza Mungu na tena ni adui wa watu wote, 16 pwakijitahidi kutuzuia tusizungumze na watu wa Mataifa ili kwamba wapate kuokolewa. Kwa njia hii wanazidi kujilundikia dhambi zao hadi kikomo. Lakini hatimaye ghadhabu ya Mungu imewafikia.

Paulo Atamani Kuwaona Wathesalonike

17 qLakini ndugu zetu, tulipotenganishwa nanyi kwa kitambo kidogo (ingawa kutengana huko kulikuwa kwa mwili tu, si kwa moyo), tulizidi kuwa na shauku kubwa kuwaona uso kwa uso. 18 rMaana tulitaka kuja kwenu, hasa mimi Paulo, nilitaka kuja tena na tena, lakini Shetani akatuzuia. 19 sKwa maana tumaini letu ni nini, au furaha yetu au taji yetu ya kujisifia mbele za Bwana Yesu Kristo wakati wa kuja kwake? Je, si ni ninyi? 20 tNaam, ninyi ndio fahari yetu na furaha yetu.

Copyright information for SwhNEN