2 Chronicles 16

Miaka Ya Mwisho Ya Mfalme Asa

(1 Wafalme 15:17-24)

1 aKatika mwaka wa thelathini na sita wa utawala wa Asa, Mfalme Baasha wa Israeli akashambulia Yuda na kuweka ngome mji wa Rama ili kumzuia yeyote asitoke wala kuingia nchi ya Mfalme Asa wa Yuda.

2Ndipo Asa akachukua fedha na dhahabu kutoka hazina ya Hekalu la Bwana na kutoka jumba lake mwenyewe la kifalme na kumpelekea Ben-Hadadi mfalme wa Aramu, ambaye alikuwa anatawala huko Dameski. 3 bAkasema, “Pawepo na mkataba kati yangu na wewe, kama ulivyokuwepo kati ya baba yangu na baba yako. Tazama, nimekuletea fedha na dhahabu. Sasa vunja mkataba wako na Baasha mfalme wa Israeli ili aniondokee mimi.”

4Ben-Hadadi akakubaliana na Mfalme Asa na kutuma majemadari wa majeshi yake dhidi ya miji ya Israeli. Wakashinda Iyoni, Dani, Abel-Maimu na miji yote ya hazina ya Naftali. 5Baasha aliposikia jambo hili, akasimamisha kujenga Rama na kuacha kazi yake. 6Ndipo Mfalme Asa akawaleta watu wote wa Yuda, nao wakachukua mawe na miti ambayo Baasha alikuwa anavitumia huko Rama. Kwa vitu hivyo akajenga Geba na Mispa.

7 cIkawa wakati huo mwonaji Hanani akamjia Mfalme Asa wa Yuda na kumwambia: “Kwa sababu ulimtegemea mfalme wa Aramu nawe hukumtegemea Bwana Mungu wako, jeshi la mfalme wa Aramu limeponyoka mkononi mwako. 8 dJe, hukumbuki lililotendeka kwa Wakushi na Walibia, hawakuwa jeshi lenye nguvu na magari mengi ya vita na wapanda farasi? Hata hivyo, ulipomtegemea Bwana yeye aliwatia mkononi mwako. 9 eKwa kuwa macho ya Bwana hukimbiakimbia duniani kote ili kujionyesha mwenye nguvu kwa ajili ya wale ambao mioyo yao inamtegemea kwa ukamilifu. Umefanya jambo la upumbavu na kuanzia sasa na kuendelea utakuwa na vita.”

10 fAsa akamkasirikia mwonaji kwa sababu ya jambo hili. Alikuwa ameghadhibika sana hata akamweka gerezani. Wakati huo huo Asa akaanza kuwatesa na kuwaonea baadhi ya watu kwa ukatili.

11Matukio ya utawala wa Asa, kuanzia mwanzo mpaka mwisho, yameandikwa katika kitabu cha wafalme wa Yuda na Israeli. 12 gKatika mwaka wa thelathini na tisa wa utawala wake, Asa alipatwa na ugonjwa kwenye miguu yake. Ingawa ugonjwa wake ulimzidia sana, hata katika kuugua kwake hakutafuta msaada kutoka kwa Bwana bali kwa matabibu tu. 13Katika mwaka wa arobaini na moja wa utawala wa Asa, alikufa na kulala na baba zake. 14 hNao wakamzika katika kaburi lile alilokuwa amejichongea mwenyewe katika Mji wa Daudi. Wakamzika kwa jeneza lililowekwa vikolezi na mchanganyiko wa manukato ya aina mbalimbali yaliyotengenezwa kwa utaalamu wa mtengeneza marashi, nao wakawasha moto mkubwa kwa heshima yake.

Copyright information for SwhNEN