2 Samuel 24

Daudi Ahesabu Wapiganaji

(1 Nyakati 21:1-27)

1 aHasira ya Bwana ikawaka tena dhidi ya Israeli, naye akamchochea Daudi dhidi yao, akisema, “Nenda ukawahesabu Israeli na Yuda.”

2 bKwa hiyo mfalme akamwambia Yoabu, pamoja na majemadari wa jeshi aliokuwa nao, “Nendeni kwa makabila yote ya Israeli kuanzia Dani hadi Beer-Sheba na mwandikishe watu wapiganaji, ili niweze kujua idadi yao.”

3 cLakini Yoabu akamjibu mfalme, “Bwana Mungu wako na azidishe jeshi mara mia, nayo macho ya bwana wangu mfalme na yaone hili. Lakini kwa nini bwana wangu mfalme anataka kufanya kitu cha namna hii?”

4 dHata hivyo, neno la mfalme likawa na nguvu juu ya Yoabu pamoja na majemadari wa jeshi, kwa hiyo wakaondoka mbele ya mfalme kuandikisha wapiganaji wa Israeli.

5 eBaada ya kuvuka Yordani, walipiga kambi karibu na Aroeri, kusini ya mji ulioko kwenye bonde jembamba, ndipo wakipitia Gadi, wakaenda hadi Yazeri. 6 fWalikwenda hadi Gileadi na pia eneo la Tahtimu-Hodshi, wakaendelea hadi Dani-Yaani na kuzunguka kuelekea Sidoni. 7 gKisha wakaenda kuelekea ngome ya Tiro pamoja na miji yote ya Wahivi na ya Wakanaani. Mwishoni, walikwenda mpaka Beer-Sheba katika Negebu ya Yuda.

8Baada ya kupita katika nchi nzima, walirudi Yerusalemu baada ya miezi tisa na siku ishirini.

9 hYoabu akatoa hesabu ya wapiganaji kwa mfalme: Katika Israeli kulikuwako watu 800,000 wenye uwezo wa kupigana, na katika Yuda watu 500,000.

10 iDhamiri ya Daudi ilishtuka baada ya kuwahesabu wapiganaji, naye akamwambia Bwana, “Nimefanya dhambi kubwa kwa kufanya jambo hili. Ee Bwana, sasa ninakusihi, ondoa hatia ya mtumishi wako. Nimefanya jambo la kipumbavu sana.”

11 jKabla Daudi hajaamka kesho yake asubuhi, neno la Bwana lilikuwa limemjia Gadi nabii, aliyekuwa mwonaji wa Daudi, kusema: 12“Nenda ukamwambie Daudi, ‘Hivi ndivyo asemavyo Bwana: Ninakupa wewe uchaguzi wa mambo matatu. Nichagulie mojawapo nitakalotenda dhidi yako.’ ”

13 kBasi Gadi akaenda kwa Daudi na kumwambia, “Je, ije njaa ya miaka mitatu katika nchi yako? Au miezi mitatu ya kukimbia adui zako wakikufuatia? Au siku tatu za tauni katika nchi yako? Basi sasa, fikiri juu ya hilo na uamue jinsi nitakavyomjibu huyo aliyenituma.”

14 lDaudi akamjibu Gadi, “Nitataabika sana. Afadhali tuangukie mikononi mwa Bwana, kwa maana rehema zake ni kuu, lakini usiniache nianguke mikononi mwa wanadamu.”

15 mBasi Bwana akatuma tauni katika Israeli kuanzia asubuhi mpaka mwisho wa muda ulioamriwa, wakafa watu 70,000 kuanzia Dani hadi Beer-Sheba. 16 nMalaika aliponyoosha mkono wake ili kuangamiza Yerusalemu, Bwana akahuzunika kwa sababu ya maafa, akamwambia yule malaika aliyekuwa anawadhuru watu, “Yatosha! Rudisha mkono wako.” Wakati huo malaika wa Bwana alikuwa kwenye sakafu ya kupuria ya Arauna,
Pia anaitwa Ornani kwa Kiebrania.
Myebusi.

17 pIkawa Daudi alipomwona huyo malaika aliyekuwa akiwaua watu, akamwambia Bwana, “Mimi ndiye niliyetenda dhambi na kukosa. Hawa ni kondoo tu. Wamefanya nini? Mkono wako uwe juu yangu na nyumba yangu.”

Daudi Ajenga Madhabahu

18 qSiku hiyo Gadi akamwendea Daudi na kumwambia, “Panda ukamjengee Bwana madhabahu kwenye sakafu ya kupuria ya Arauna Myebusi.” 19Kwa hiyo Daudi akakwea kama vile Bwana alivyokuwa ameamuru kwa kinywa cha Gadi. 20Arauna alipotazama na kumwona mfalme na watu wake wakija kumwelekea, alitoka nje na kusujudu mbele ya mfalme kifudifudi, akiuinamisha uso wake ardhini.

21 rArauna akasema, “Mbona bwana wangu mfalme amekuja kwa mtumishi wake?”

Daudi akajibu, “Kununua sakafu yako ya kupuria, ili niweze kumjengea Bwana madhabahu, ili tauni iliyo katika watu iondolewe.”

22 sArauna akamwambia Daudi, “Bwana wangu mfalme na achukue chochote kinachompendeza na akitoe sadaka. Hapa kuna maksai kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, pia kuna miti ya kupuria na nira za ngʼombe kwa ajili ya kuni. 23 tEe mfalme, Arauna anatoa vyote hivi kwa mfalme.” Pia Arauna akamwambia mfalme, “Bwana Mungu wako na akukubali.”

24 uLakini mfalme akamjibu Arauna, “La hasha, nasisitiza kuvilipia. Sitatoa sadaka ya kuteketezwa kwa Bwana Mungu wangu isiyonigharimu chochote.”

Kwa hiyo Daudi akanunua ile sakafu ya kupuria nafaka na maksai, akazilipia shekeli hamsini za fedha.
Shekeli 50 za fedha ni sawa na gramu 600.
25 wKisha Daudi akamjengea Bwana madhabahu mahali hapo, na kutoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani. Kisha Bwana akajibu kwa ajili ya nchi, nayo tauni ikakoma katika Israeli.

Copyright information for SwhNEN