Hebrews 3

Yesu Ni Mkuu Kuliko Mose

1 aKwa hiyo ndugu watakatifu, mnaoshiriki mwito wa mbinguni, mtafakarini Yesu, mtume na Kuhani Mkuu wa ukiri wetu. 2 bAlikuwa mwaminifu kwa yeye aliyemweka, kama vile Mose alivyokuwa mwaminifu katika nyumba yote ya Mungu. 3 cYesu ameonekana anastahili heshima kubwa kuliko Mose, kama vile mjenzi wa nyumba alivyo wa heshima kubwa kuliko nyumba yenyewe. 4 dKwa kuwa kila nyumba hujengwa na mtu fulani, lakini Mungu ni mjenzi wa kila kitu. 5 eBasi Mose kama mtumishi alikuwa mwaminifu katika nyumba yote ya Mungu, akishuhudia kwa yale ambayo yangetamkwa baadaye. 6 fLakini Kristo ni mwaminifu kama Mwana katika nyumba ya Mungu. Sisi ndio nyumba yake, kama tutashikilia sana ujasiri wetu na tumaini tunalojivunia.

Onyo Dhidi Ya Kutokuamini

7 gKwa hiyo, kama Roho Mtakatifu asemavyo:

“Leo, kama mkiisikia sauti yake,
8 hmsiifanye mioyo yenu migumu,
kama mlivyofanya katika uasi,
wakati ule wa kujaribiwa jangwani,
9 iambapo baba zenu walinijaribu na kunipima
ingawa kwa miaka arobaini
walikuwa wameyaona matendo yangu.
10Hiyo ndiyo sababu nilikasirikia kizazi kile,
nami nikasema, ‘Siku zote mioyo yao imepotoka,
nao hawajazijua njia zangu.’
11 jHivyo nikatangaza kwa kiapo katika hasira yangu,
‘Kamwe hawataingia rahani mwangu.’ ”
12 kNdugu zangu, angalieni, asiwepo miongoni mwenu mtu mwenye moyo mwovu usioamini, unaojitenga na Mungu aliye hai. 13 lLakini mtiane moyo mtu na mwenzake kila siku, maadamu iitwapo Leo, ili asiwepo hata mmoja wenu mwenye kufanywa mgumu kwa udanganyifu wa dhambi. 14 mKwa kuwa tumekuwa washiriki wa Kristo, kama tukishikamana tu kwa uthabiti na tumaini letu la kwanza hadi mwisho. 15 nKama ilivyonenwa:

“Leo, kama mkiisikia sauti yake,
msiifanye mioyo yenu migumu
kama mlivyofanya wakati wa kuasi.”
16Basi ni nani waliosikia lakini bado wakaasi? Je, si wale wote waliotoka Misri wakiongozwa na Mose? 17Lakini ni nani aliowakasirikia miaka arobaini? Je, si wale waliofanya dhambi ambao miili yao ilianguka jangwani? 18Ni nani hao ambao Mungu aliapa kuwa kamwe hawataingia rahani mwake isipokuwa ni wale waliokataa kutii? 19Hivyo tunaona kwamba hawakuweza kuingia kwa sababu ya kutokuamini kwao.

Copyright information for SwhNEN