Isaiah 12

Kushukuru Na Kusifu

1 aKatika siku ile utasema:

“Nitakusifu wewe, Ee Bwana.
Ingawa ulinikasirikia,
hasira yako imegeukia mbali
nawe umenifariji.
2 bHakika Mungu ni wokovu wangu;
nitamtumaini wala sitaogopa.
Bwana, Bwana, ni nguvu zangu na wimbo wangu;
amekuwa wokovu wangu.”
3 cKwa furaha mtachota maji
kutoka visima vya wokovu.
4 dKatika siku hiyo mtasema:

“Mshukuruni Bwana, mliitie jina lake;
julisheni miongoni mwa mataifa yale aliyoyafanya,
tangazeni kuwa jina lake limetukuka.
5 eMwimbieni Bwana, kwa kuwa ametenda mambo makuu,
hili na lijulikane duniani kote.
6 fPazeni sauti mwimbe kwa furaha, watu wa Sayuni,
kwa maana mkuu ni yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli miongoni mwenu.”
Copyright information for SwhNEN