Isaiah 3

Hukumu Juu Ya Yerusalemu Na Yuda.

1 aTazama sasa, Bwana,
Bwana Mwenye Nguvu Zote,
yu karibu kuwaondolea Yerusalemu na Yuda
upatikanaji wa mahitaji na misaada,
upatikanaji wote wa chakula na tegemeo lote la maji,
2 bshujaa na mtu wa vita,
mwamuzi na nabii,
mwaguzi na mzee,
3 cjemadari wa kikosi cha watu hamsini
na mtu mwenye cheo, mshauri,
fundi stadi na mlozi mjanja.

4 dNitawafanya wavulana wawe maafisa wao,
watoto ndio watakaowatawala.
5 eWatu wataoneana wao kwa wao:
mtu dhidi ya mtu, na jirani dhidi ya jirani yake.
Kijana atainuka dhidi ya mzee,
mtu mnyonge dhidi ya mtu mwenye heshima.

6Mtu atamkamata mmoja wa ndugu zake
katika nyumba ya baba yake na kusema,
“Unalo joho, sasa uwe kiongozi wetu,
tawala lundo hili la magofu!”
7 fLakini siku hiyo atapiga kelele akisema,
“Sina uponyaji.
Sina chakula wala mavazi katika nyumba yangu,
msinifanye niwe kiongozi wa watu.”

8 gYerusalemu inapepesuka,
Yuda inaanguka;
maneno yao na matendo yao ni kinyume na Bwana,
wakiudharau uwepo wake uliotukuka.
9 hNyuso zao zinavyoonekana zinashuhudia dhidi yao,
hujivunia dhambi yao kama Sodoma,
wala hawaifichi.
Ole wao!
Wamejiletea maafa juu yao wenyewe.

10 iWaambie wanyofu itakuwa heri kwao,
kwa kuwa watafurahia tunda la matendo yao.
11 jOle kwa watu waovu! Maafa yapo juu yao!
Watalipwa kwa ajili ya yale mikono yao iliyotenda.

12 kVijana wanawatesa watu wangu,
wanawake wanawatawala.
Enyi watu wangu, viongozi wenu wanawapotosha,
wanawapoteza njia.

13 l Bwana anachukua nafasi yake mahakamani,
anasimama kuhukumu watu.
14 m Bwana anaingia katika hukumu
dhidi ya wazee na viongozi wa watu wake:
“Ninyi ndio mlioharibu shamba langu la mizabibu,
mali zilizonyangʼanywa maskini zimo nyumbani mwenu.
15 nMnamaanisha nini kuwaponda watu wangu
na kuzisaga nyuso za maskini?”
asema Bwana, Bwana Mwenye Nguvu Zote.

16 o Bwana asema,
“Wanawake wa Sayuni wana kiburi,
wanatembea na shingo ndefu,
wakikonyeza kwa macho yao,
wanatembea kwa hatua za madaha,
wakiwa na mapambo ya njuga kwenye vifundo vya miguu yao.
17 pKwa hiyo Bwana ataleta majipu kwenye vichwa vya wanawake wa Sayuni;
Bwana atazifanya ngozi za vichwa vyao kuwa vipara.”
18 qKatika siku ile Bwana atawanyangʼanya uzuri wao: bangili, tepe za kichwani, mikufu yenye alama za mwezi mwandamo, 19 rvipuli, vikuku, shela, 20 svilemba, mikufu ya vifundo vya miguu, mshipi, chupa za manukato na hirizi, 21 tpete zenye muhuri, pete za puani, 22 umajoho mazuri, mitandio, mavazi, kifuko cha kutilia fedha, 23 vvioo, mavazi ya kitani, taji na shali.

24 wBadala ya harufu ya manukato kutakuwa na uvundo;
badala ya mishipi, ni kamba;
badala ya nywele zilizotengenezwa vizuri, ni upara;
badala ya mavazi mazuri, ni nguo za magunia;
badala ya uzuri, ni alama ya aibu kwa chuma cha moto.
25 xWanaume wako watauawa kwa upanga,
nao mashujaa wako watauawa vitani.
26 yMalango ya Sayuni yataomboleza na kulia,
ataketi mavumbini akiwa fukara.
Copyright information for SwhNEN