Isaiah 52

1 aAmka, amka, ee Sayuni,
jivike nguvu.
Vaa mavazi yako ya fahari,
ee Yerusalemu, mji mtakatifu.
Asiyetahiriwa na aliye najisi
hataingia kwako tena.
2 bJikungʼute mavumbi yako,
inuka, uketi kwenye kiti cha enzi, ee Yerusalemu.
Jifungue minyororo iliyo shingoni mwako,
ee Binti Sayuni uliye mateka.
3 cKwa kuwa hili ndilo asemalo Bwana:

“Mliuzwa pasipo malipo,
nanyi mtakombolewa bila fedha.”
4 dKwa maana hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi:

“Hapo kwanza watu wangu walishuka Misri kuishi,
hatimaye, Ashuru wakawaonea.
5 e“Basi sasa nina nini hapa?” asema Bwana.

“Kwa kuwa watu wangu wamechukuliwa pasipo malipo,
nao wale wanaowatawala wanawadhihaki,”
asema Bwana.
“Mchana kutwa
jina langu limetukanwa bila kikomo.
6 fKwa hiyo watu wangu watalijua Jina langu;
kwa hiyo katika siku ile watajua
kwamba ndimi niliyetangulia kulisema.
Naam, ni mimi.”

7 gTazama jinsi miguu ya wale waletao habari njema
ilivyo mizuri juu ya milima,
wale wanaotangaza amani,
wanaoleta habari njema,
wanaotangaza wokovu,
wauambiao Sayuni,
“Mungu wako anatawala!”
8 hSikiliza! Walinzi wako wanapaza sauti zao,
pamoja wanapaza sauti zao kwa furaha.
Wakati Bwana atakaporejea Sayuni,
wataliona kwa macho yao wenyewe.
9 iPazeni sauti ya nyimbo za furaha pamoja,
enyi magofu ya Yerusalemu,
kwa maana Bwana amewafariji watu wake,
ameikomboa Yerusalemu.
10 jMkono mtakatifu wa Bwana umefunuliwa
machoni pa mataifa yote,
nayo miisho yote ya dunia itaona
wokovu wa Mungu wetu.

11 kOndokeni, ondokeni, tokeni huko!
Msiguse kitu chochote kilicho najisi!
Tokeni kati yake mwe safi,
ninyi mchukuao vyombo vya Bwana.
12 lLakini hamtaondoka kwa haraka,
wala hamtakwenda kwa kukimbia;
kwa maana Bwana atatangulia mbele yenu,
Mungu wa Israeli atakuwa mlinzi nyuma yenu.

Mateso Na Utukufu Wa Mtumishi

13 mTazama, mtumishi wangu atatenda kwa hekima;
atatukuzwa, na kuinuliwa juu, na kukwezwa sana.
14 nKama walivyokuwa wengi
walioshangazwa naye,
kwani uso wake ulikuwa umeharibiwa sana
zaidi ya mtu yeyote
na umbo lake kuharibiwa
zaidi ya mfano wa mwanadamu:
15 ohivyo atayashangaza mataifa mengi,
nao wafalme watafunga vinywa vyao kwa sababu yake.
Kwa kuwa yale ambayo hawakuambiwa, watayaona,
nayo yale wasiyoyasikia, watayafahamu.
Copyright information for SwhNEN