Isaiah 53

1 aNi nani aliyeamini ujumbe wetu,
na mkono wa Bwana umefunuliwa kwa nani?
2 bAlikua mbele yake kama mche mwororo
na kama mzizi katika nchi kavu.
Hakuwa na uzuri wala utukufu wa kutuvutia kwake,
hakuwa na chochote katika sura yake cha kutufanya tumtamani.
3 cAlidharauliwa na kukataliwa na wanadamu,
mtu wa huzuni nyingi, ajuaye mateso.
Kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao,
alidharauliwa, wala hatukumhesabu kuwa kitu.

4 dHakika alichukua udhaifu wetu
na akajitwika huzuni zetu,
hata hivyo tulidhania kuwa amepigwa na Mungu,
akapigwa sana naye, na kuteswa.
5 eLakini alitobolewa kwa ajili ya makosa yetu,
alichubuliwa kwa ajili ya maovu yetu;
adhabu iliyotuletea sisi amani ilikuwa juu yake,
na kwa majeraha yake sisi tumepona.
6 fSisi sote, kama kondoo, tumepotea,
kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe,
naye Bwana aliweka juu yake
maovu yetu sisi sote.

7 gAlionewa na kuteswa,
hata hivyo hakufungua kinywa chake;
aliongozwa kama mwana-kondoo
apelekwaye machinjoni,
kama vile kondoo anyamazavyo mbele ya wao wamkataye manyoya,
hivyo hakufungua kinywa chake.
8 hKwa kuonewa na kuhukumiwa aliondolewa.
Nani awezaye kueleza kuhusu kizazi chake?
Kwa maana alikatiliwa mbali na nchi ya walio hai,
alipigwa kwa ajili ya makosa ya watu wangu.
9 iWakamfanyia kaburi pamoja na waovu,
pamoja na matajiri katika kifo chake,
ingawa hakutenda jeuri,
wala hapakuwa na hila kinywani mwake.

10 jLakini yalikuwa ni mapenzi ya Bwana
kumchubua na kumsababisha ateseke.
Ingawa Bwana amefanya maisha yake
kuwa sadaka ya hatia,
ataona uzao wake na kuishi siku nyingi,
nayo mapenzi ya Bwana yatafanikiwa mkononi mwake.
11 kBaada ya maumivu ya nafsi yake,
ataona nuru ya uzima na kuridhika;
kwa maarifa yake, mtumishi wangu mwenye haki
atawafanya wengi kuwa wenye haki,
naye atayachukua maovu yao.
12 lKwa hiyo nitamgawia sehemu miongoni mwa wakuu,
naye atagawana nyara pamoja na wenye nguvu,
kwa sababu aliyamimina maisha yake hadi mauti,
naye alihesabiwa pamoja na wakosaji.
Kwa kuwa alichukua dhambi za wengi,
na kuwaombea wakosaji.
Copyright information for SwhNEN